SIKU moja baada ya kundi la vijana wanaoaminika kuwa wanachama
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwacharanga mapanga wafuasi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji
Peter Msigwa, sasa ametishiwa kuuawa.
Habari zinasema kuwa Diwani wa Kata ya Nduli, Idd Rashid Chonanga,
jana asubuhi alimvamia Mchungaji Msigwa ofisini kwake na kumtaka ajue
kuwa siku zake zinahesabika, hata kama juzi alinusurika, lakini
atahakikisha ameuawa kwa njia zozote zile, hali iliyomfanya Mbunge huyo
kukimbilia polisi kuomba msaada.
Diwani huyo, ndiye anayetuhumiwa kusimamia kikamilifu tukio la
kucharangwa mapanga kwa wafuasi watatu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) wakati wa mkutano wa Mbunge huyo uliofanyika katika
uwanja wa kata ya Nduli na kuwajeruhi vibaya.
Katika mkutano huo ambao ulifanywa na Mbunge huyo, mwenyekiti, katibu,
wajumbe sita wa CCM wa kata ya Nduli na wanachama wengine takriban 90
walihamia CHADEMA, huku ikidaiwa kuwa wengine zaidi ya 150 wangelikihama
chama tawala wiki hii.
Akizungumza akiwa polisi, Mchungaji Msigwa alisema kuwa kauli ya
diwani huyo imemtisha kwa kuwa anajua ina baraka za viongozi wake wa
ngazi ya juu.
Mchungaji Msigwa alilitaka Jeshi la Polisi lisifanye mzaha katika
jambo hilo, kwa kile alichodai kuwa ni jambo la hatari na lenye lengo
mahsusi la kuwatisha viongozi wa vyama vya upinzani na wananchi baada ya
kuona kuwa CCM inazidi kupoteza maelfu ya wanachama wake kila kukicha.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, alisema hadi muda
huo alikuwa hajapokea taarifa hizo, lakini akaahidi kulishughulikia
jambo hilo kikamilifu, ili kulinda amani na usalama wa kiongozi huyo na
raia wengine.
Hata hivyo, Tanzania Daima imethibitishiwa kukamatwa kwa diwani huyo
na vijana wa CCM waliohusika kuwakata mapanga watu watatu waliokuwa
katika mkutano wa Mbunge huyo juzi.
Mmoja wa maafisa wa polisi alidai kuwa miongoni mwa vijana
waliokamatwa, wawili ni watoto wa diwani huyo na kwamba watu wengine
wanne, akiwemo mfanyakazi wa diwani huyo, bado wanasakwa na jeshi hilo
kwa kuhusiana na tukio la juzi.
Akizungumzia kutishwa kwa maisha kwa Mbunge Msigwa, aliyekuwa
mwenyekiti wa CCM kata ya Nduli, Ayub Mwenda, alisema tangu jana amekuwa
akipokea vitisho na kudai kuwa hali hiyo haitakisadia chama tawala,
badala yake kinasababisha kichukiwe na hata na wale waliokuwa
wakikipenda.
“Wananchi wengi wamechukizwa sana na tukio la juzi, na wakisikia tena
na hili alilofanya huyu diwani leo, ndio itakuwa imezidi kujipalia mkaa.
Hii ni nchi ya demokrasia ya vyama vingi, na kila mtu anayo haki ya
kujiunga na chama chochote, sasa inashangaza kuona inakuwa nongwa kwao,”
alisema Mwenda alipohojiwa na gazeti hili.
Wakati huohuo, mmoja wa watu waliojeruhiwa vibaya katika shambulizi la
mapanga juzi, Osca Sanga bado amelazwa katika hospitali ya mkoa, wakati
wengine wawili waliruhusiwa jana.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, George Kabona, amesema Sanga
anaendelea na matibabu, ingawa alikiri kuwa hali yake bado haijawa ya
kuridhisha.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment