Tuesday, May 15, 2012

Katibu Chadema adaiwa kunyofoa sikio la kijana gesti


Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa wilaya ya Ilemela jijini Mwanza, Abel Mwesa,  anatuhumiwa kumng’ata sikio kijana wa Mtaa wa Nyambiti, baada ya kunyimwa chumba cha kulala na mpenzi wake.
 
Inadaiwa kuwa, kiongozi huyo wa Chadema alikwenda katika nyumba hiyo ya kulala wageni kwa lengo la kwenda kufanya mapenzi.
 
Nyumba hiyo ya kulala wageni (gesti) inajulikana kwa jina la Amani, na ipo katika mtaani Nyambiti.
 
Mwesa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa huo, anadaiwa kumng’ata sikio Razaro Norbert (25) saa 5 usiku, Aprili 26 mwaka huu.
 
Kituo cha televisheni cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), jana saa mbili usiku kilionesha namna kijana alivyonyofolewa sikio la kulia.

 Inadaiwa kuwa, tukio hilo limeripotiwa kituo cha polisi cha Nyakato, na kwamba, mtuhumiwa huyo,anayedaiwa kujiita Rais wa Mtaa wa Nyambiti, hajakamatwa.
 
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo, ameagiza Mwesa akamatwe.

Akisimulia mkasa huo jana ofisini kwa Mkuu wa mkoa, Norbert alidai kwamba, siku ya tukio mkasa ulianza baada ya kukataa kumpa Mwesa chumba cha kulala wakati akiwa na mwanamke aliyedai ni mpenzi wake.

“Nilimwambia mimi siyo mhudumu wa gesti hiyo hapo, nafanya biashara ndogondogo tu, akachukia sana na kuanza kufoka kuwa yeye ndiye Rais wa Mtaa huo ntamnyimaje chumba, ndipo akapiga simu kwa 'makamanda' wake wawili wakaja kunikamata na kuanza kunipa kipigo.” Alieleza.

Alidai kuwa, wakati wakimshushia kipigo, Mwesa alimshika kwa hasira na kumng’ata sikio la kulia na kuliondoa lote.
 
Sehemu iliyoathirika jana ilikuwa inavuja usaha, na kwa mujibu wa Norbert, alitibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Kijana huyo alidai kwa Mkuu wa Mkoa kwamba, pamoja na kuripoti katika kituo cha polisi cha Mwatex siku hiyo (NY/RB/3059/2012) na kupatiwa PF3 kwa ajili ya matibabu, hadi jana, mtuhumiwa alikuwa hajakamatwa na kwamba, askari wa kituo hicho wakizidi kumshinikiza apewe fidia ya shilingi 200,000/= na kuachana na kesi hiyo.

Amedai kuwa, tangu wakati huo amekuwa akipewa vitisho kwa maneno kuwa atauawa, na ameandikiwa barua iliyochorwa kaburi (tunayo).
 
Norbert amemuonyesha Mkuu wa mkoa barua hiyo.


Wakati anatoa agizo la kukamatwa kwa Mwesa Ndikilo alisema “Kituo cha Mwatex kinamaslahi na Mwesa ambaye anadaiwa kujiita Rais wa Mtaa huo anaweza kuamuru hata maduka yafungwe"

No comments:

Post a Comment