Tuesday, May 29, 2012

Lulu ana umri wa miaka mingapi?

  Elizabeth Michael 'Lulu'  akiwasili katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusikilizwa kwa shauri la ufafanuzi kuhusu wake.

Lulu anakabiliwa na mashitaka ya kusababisha kifo cha aliyekuwa mcheza filamu nyota nchini Steven Charles Kanumba aliyekufa usiku wa kuamkia Aprili 7 mwaka huu Sinza Vatican Jijini Dar es Salaam.

Picha zote kwa hisani ya blog ya Francis Dande
Lulu akiwa mahakamani jana

MAWAKILI wa Serikali katika kesi ya mauaji inayomkabili mwigizaji wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’, wamepinga maombi ya kuuchunguza umri  wa mshitakiwa huyo.

 Mawakili wanaomtetea Lulu wameiomba Mahakama Kuu ichunguze umri wa msanii huyo au kuiamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ifanye hivyo.

Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro ameiomba Mahakama hiyo isisikilize maombi ya Lulu kwa madai kwamba yaliwasilishwa mahakamani hapo kimakosa, na pia sheria iliyotumika ina kasoro.

Sheria iliyotumiwa na mawakili wa utetezi ni Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, kifungu cha 113 inayoruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa umri wa mshitakiwa.

Kimaro amedai kuwa, maombi hayo yalikwishatolewa  katika Mahakama ya Kisutu na ‘kugonga mwamba’ na kuongeza kuwa mawakili wa utetezi walitakiwa kuukatia rufaa uamuzi huo au kuomba mapitio yake, lakini si kuwasilisha maombi mapya.

  Kimaro aliyekuwa akisaidiwa na Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alidai kuwa maombi ya pili kwa Mahakama hiyo ya kusitisha kesi ya Kisutu ni batili.

Alidai ubatili huo ni kwa sababu kesi ya Lulu Kisutu haisikilizwi, iko katika hatua ya uchunguzi na sheria inataka kesi kusimama ikiwa katika hatua ya kusikilizwa.

  Mawakili wa Lulu, Peter Kibatala, Fulgence Masawe na Kennedy Fungamtama na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Joaquine De- Melo aliyetambulishwa kama mtazamaji, walipinga.

Mawakili hao walidai kuwa waliwasilisha maombi yao mahakamani hapo kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu uliotamka kama kuna maombi yoyote yawasilishwe katika Mahakama hiyo.

Walidai kuwa Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kutoa uamuzi wa maombi yao kwa mujibu wa sheria na hakuna walipokosea na kuiomba Mahakama ipuuze maombi ya mawakili wa Serikali.

No comments:

Post a Comment