Thursday, December 8, 2011

Hazina-Tunaheshimu kauli ya Makinda

Naibu Waziri wa Fedha, Gregory Theu amesema, Hazina wanaheshimu kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba wabunge wamenza kulipwa posho mpya 200,000/- kwa kila kikao cha Bunge.


Theu alitoa msimamo huo jana katika viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaaam alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa maonesho ya miaka 50 ya uhuru.


“Spika kama kasema zimeanza kulipwa sisi hatuna cha kusema. Iwapo wameanza kulipwa ama bado sisi sio jukumu letu hilo na tutaheshimu kauli hiyo na si vinginevyo,” alisema Theu.


Utata wa kauliJuzi sakata hilo la posho lilichukua sura mpya, baada ya Spika Makinda, kutangaza kuwa wabunge wameshaanza kulipwa viwango vipya vya Sh200,000 badala ya Sh 70,000 za awali, akipingana na Katibu wake, Dk Kashililah, aliyekanusha wabunge kuanza kulipwa.


Wakati Dk Kashililah akitoa taarifa rasmi kukanusha taarifa za wabunge kuongezewa posho hizo, Makinda juzi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa tayari posho hizo zimeanza kulipwa.


"Mbunge huyu alikuwa anapata Sh 70,000 kwa hiyo tumemwongezea 130,000 na hupati unless (isipokuwa) umefanya kazi ya Bunge na amesaini asubuhi na jioni. Hujafanya hivyo hupati hizo hela,"alisema Makinda.


Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti taarifa za ndani kwamba posho za wabunge zimepanda kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 hivyo kufanya bajeti ya posho hizo kwa mwaka kufikia Sh28 bilioni.


Kutokana na ongezeko hilo, taarifa hizo zilisema kila mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 kama posho ya kujikimu (per diem) anapokuwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao (sitting allowance) Sh200,000 na mafuta ya gari Sh50,000 kila siku, sawa na Sh330,000 kwa siku huku mshahara jumla kabla ya makato ni Sh2.3 milioni na ukikatwa unabaki Sh 1.7milioni.


Wakati taarifa hiyo inaripotiwa, Dk Kashililah alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu yeye si msemaji wa Bunge na akashauri atafutwe Spika wa Bunge. 




Lakini, baada ya mjadala wa takriban juma moja wa wanaharakati, wabunge na wasomi kupinga nyongeza hiyo ya posho, Dk Kashililah aliibuka na kukiri kuwa wabunge wanataka waongezewe posho za vikao, lakini mapendekezo hayo, hayajaanza kutekelezwa.


Kwa mujibu wa Katibu huyo Bunge, mapendekezo ya kutaka posho za wabunge zipande, yaliibuka katika mkutano wa wabunge mjini Dodoma Novemba 8 mwaka huu, lakini hadi sasa hayajaanza kutekelezwa.


"Suala la mabadiliko ya posho za vikao vya Bunge lilijitokeza katika Mkutano wa wabunge, Novemba 8, 2011 walipoiomba Serikali iangalie upya suala hilo kwa lengo la kuboresha,” alisema Dk Kashililah katika taarifa hiyo.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment