Thursday, December 8, 2011

Mbatia- Mfumo wa utoaji posho wa kifisadi

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema, mfumo wa utoaji wa posho nchini ni wa kifisadi.



Mbatia alisema kuwa kuna haja ya kuutizama upya mfumo huo ambao umeacha pengo kubwa kati ya mwenye nacho na asiyekua nacho.Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alisema suala la kupishana kauli kwa viongozi wawili wa taasisi moja, ni udhaifu mkubwa kwa taasisi hiyo.



“Suala la posho inatakiwa litazamwe upya katika mihimili yote ya dola, panapokuwa hakuna kanuni ya kuweka uwiano miongoni mwa mihimili hii, ”alisema Kafulila na kuongeza.



“Inatakiwa itazamwe upya, hili suala la posho lipatiwe ufumbuzi kabisa, ukiangalia huko serikalini kuna mashirika ya umma ambayo wanalipa posho za Sh400,000 mpaka 500,000, mishahara wanalipa Sh10milioni mpaka 15 milioni,” alisema Kafulila:



Profesa Ruth Meena alisema ni jambo la kusikitisha kuwa viongozi wa Bunge wanapishana kauli juu ya suala hilo la posho.



“Inasikitisha sana hawa wawakilishi wetu kujiongezea posho wakisema kuwa gharama za maisha zimepanda, kwenye hali kama hii ya sasa hakuna njia yeyote utakayoweza kutumia kuhalalisha ongezeka kama hili,” alisema Profesa Meena.



Dk Biassio Ndenjenje kutoka Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT) alisema, ingekuwa vyema fedha hizo za kuwalipa wabunge posho, zikatumika kwa ajili ya kutatua matatizo ya sekta ya elimu na afya kuliko kuwaongezea wabunge posho.



Taasisi ya Kimataifa ya JDPA Foundation (JPF), inayoendesha Kituo cha Haki za Binadamu, Demokrasia na Utawala Bora Afrika, imetishia kuitisha maandamano yasiyokuwa na kikomo nchi nzima kuanzia Disemba 15 kupinga posho hizo.



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Praygod Mmassy alisema wamechukua hatua hiyo kutokana na wabunge kujiongezea posho huku wananchi wakiwa wanaishi maisha magumu.



Baadhi ya wananchi nao walikuwa na maoni tofauti ambapo Prisca John wa jijini Dar es Salaam alisema, kuongezwa kwa posho za wabunge kunadhihirisha wazi jinsi ufisadi ulivyokithiri kwa baadhi ya watendaji ambao alidai wanajitizama wenyewe kuliko kutazama wananchi waliowachagua.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment