Thursday, December 8, 2011

Viongozi wa dini, wanaharakati wapinga posho mpya za wabunge

NYONGEZA ya posho za vikao iliyothibitishwa juzi na Spika Anne Makinda kwamba imeanza kutolewa Bunge lililopita, imeleta balaa.


Wabunge, wasomi, wanaharakati na viongozi wa dini, wanapinga ongezeko hilo na wanamtaka Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kuwajibika kwa kile walichoeleza kuwa ameudanganya umma.


Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti kuhusu posho hizo ambazo Serikali katika Mpango wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliopitishwa katika Bunge la Bajeti, ilitangaza kuzipunguza, watu hao wa kada tofauti walishangaa uamuzi huo mpya wa Bunge kuziongeza.


Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema ongezeko hilo linatakiwa kusitishwa kwa kuwa mchakato wake umefanyika kinyume na taratibu na kwamba halina uhalali wala halijazingatia uhalisia wa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi.


Mnyika alifafanua kwamba kauli ya Spika Makinda kwamba nyongeza hiyo inatokana na kupanda kwa gharama za maisha mkoani Dodoma haina ukweli, wala mantiki na ina mwelekeo wa upendeleo. Akamtaka Rais Jakaya Kikwete kutolea kauli kuhusu jambo hilo.


Alisema utetezi wa Spika Makinda kuhalalisha kupandishwa kwa posho hizo, hauna maana na kwamba kama sababu ingekuwa kupanda kwa gharama ya maisha, ingepandishwa posho ya kujikimu (subsistence allowance) ambayo imebaki pale pale Sh 80,000.


Mnyika alisema alikuwepo kwenye mkutano wa Novemba 8, 2011 na hakuna uamuzi wowote ambao ulifikiwa wa kuiomba Serikali ipandishe posho za vikao na yenyewe.


Alisema kilichotokea siku hiyo ni kwamba katika kuchangia maelezo ya Serikali na ya Bunge kuhusu masuala mbalimbali yaliyojiri baada ya mkutano wa nne wa Bunge na mpangilio wa Mkutano wa Tano wa Bunge, wabunge walipewa fursa ya kujadili taarifa hizo.


Alisema wabunge hawajawahi kupatiwa nakala ya muhtasari au kumbukumbu za vikao vya Kamati ya Uongozi au vya Tume ya Bunge ambavyo vimekaa na kupitisha nyongeza ya posho ya vikao kutoka Sh70,000 mpaka Sh200,000, kama Spika alivyonukuliwa na vyombo vya habari.


Viongozi wa dini wanenaAskofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilani alisema ongezeko hilo la posho limekuja ghafla na kwamba kiwango hicho ni kikubwa na hakiendani na hali halisi ya uchumi wa nchi.


“Watanzania wengi wanalalamika maisha magumu sasa wabunge wanapoongezewa posho kwa kiwango kinachofikia Sh 200,000 watambue kwamba kuna wananchi wanaohitaji msaada, hizo nyongeza za posho zingeweza kuwasaidia kwa namna moja ama nyingine ambapo ongezeko la posho hizo zingeweza kuwasaidia” alisema Kilaini.


Kwa upande wake, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Alhad Mussa Salumu alisema kwamba haoni tatizo posho za wabunge kuongezeka na kwamba kutokana na majukumu yao mazito ya kuwahudumia wananchi.


“Ni jambo jema, lakini wabunge watambue kwamba wananchi waliowachagua wana matatizo mengi ya kiuchumi sasa wanaposikia wabunge wameongezewa posho lazima nao watahoji, lakini kinachotakiwa ni kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kutatua matatizo ya wananchi wao,”alisema Alhad Salumu.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment