Thursday, December 1, 2011

Chadema: Rais Kikwete 'katuzuga', tunasusa

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011, kimekiuka makubaliano yao, hivyo kimeamua kususia mchakato mzima wa kuratibu maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia sheria hiyo.


Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa hatua hiyo imefikiwa ili kuonyesha kutoridhishwa na namna kiongozi huyo wa nchi, alivyowachezea akili.


"Kitendo cha Rais Kikwete kuusaini muswada huo bila ya kuupitia ni kinyume na makubaliano, jambo ambalo linatufanya tususie mchakato mzima wa kuuratibu maoni ya kwa ajili ya Katiba Mpya kupitia sheria ailiyoisaini,"alisema Mnyika na kuendelea:


“Tumeamua kujitoa kwenye mchakato mzima wa kuratibu Marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Katiba kutokana na Rais kukiuka makubaliano yetu Ikulu yaliyomtaka aupitie kwanza kabla ya kuusaini.”


Mnyika aliendelea kueleza kuwa Chadema iliwasilisha waraka wa mapendekezo sita kwa Rais ikiwa ni pamoja na kumtaka asiusaini muswada huo kutokana na wananchi kutoshirikishwa ipasavyo kwenye mchakato wa ukusanyaji wa maoni.


Alisema mapendekezo mengine ni uundaji wa tume huru, upatikanaji wa uwakilishi kutoka pande zote mbili za Muungano; Zanzibar na Bara ili kutoa fursa ya kupata maoni yao katika marekebisho hayo.


"Suala la tatu ni uundaji wa Bunge la Katiba na kupunguza mamlaka ya Rais na jambo la nne ni nafasi ya Zanzibar katika Muungano pamoja na mfumo mzima wa uwakilishi wa pamoja katika muundo wa Bunge la Katiba."


Mnyika alisema kutokana na hali hiyo iliyojitokeza ya Rais kutowasikiliza, watawasilisha waraka huo waliompa, kwa wananchi ili nao wausome na kutoa maoni yao.


Alisema katika kutekeleza mkakati huo, hawatafanya maandamano yeyote, isipokuwa watatoa elimu sahihi kwa wananchi juu ya Katiba wanayopaswa kuwa nayo.


“Nia yetu ni mzuri, lengo ni kuboresha upatikanaji wa Katiba iwe bora na itakayoweza kutoa nafasi ya ushiriki wa pande zote. Lakini kinachofanyika sasa ni kinyume. Tumeamua kuwarudishia wananchi wenyewe ili waweze kuamua kama tumekosea au la,”alieleza.


Tamko hilo la Chadema limekuja siku moja baada ya Rais Kikwete kutia saini muswada huo hivyo kuufanya kuwa sheria.


Rais Kikwete alitia saini muswada huo ikiwa ni siku moja baada ya yeye na viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe kukubaliana kwamba ipo haja ya kuendelea kuuboresha muswada ili ukidhi mahitaji ya kuaminiana na muafaka wa kitaifa.


Pia, walikubaliana yawepo mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment