Thursday, December 1, 2011

Jerry Muro- Waandishi fichueni maovu, msiogope

Jerry Muro baada ya kuachiwa huru jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.



ALIYEKUWA mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro na wenzake wawili, wameachiwa huru katika kesi iliyokuwa ikiwakabili ya kuomba rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage.



Akiwa nje ya Mahakama jana baada ya kuachiwa huru, Muro alisema amesamehe wabaya wake walioshiriki kutaka kumwangamiza akiwataja kuwa ni pamoja na baadhi ya vigogo serikalini na maofisa wa Jeshi la Polisi.




Awali akisoma hukumu iliyochukua takribani saa 1.30, Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Frank Moshi alisema anawaachia washitakiwa Muro, Edmond Kapama na Deogratius Mgasa, kwa sababu mashitaka yote matatu yaliyokuwa yakiwakabili, hayakuthibitishwa dhidi yao.



Alisema baada ya kuangalia ushahidi wa upande wa mashitaka na wa utetezi, Mahakama ilikuwa na maswali ya kujiuliza, ambayo ni kama upande wa mashitaka ulithibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa pasi shaka.



Aidha, Hakimu alisema kwa kuanzia na mashitaka ya kwanza ya kula njama kwa nia ya kuomba rushwa, ambayo yaliwahusu wote, Mahakama ilirejea kwenye ushahidi na hasa wa shahidi wa tatu, ambaye alikuwa mlalamikaji wa kesi hiyo, Wage.



Alisema shahidi huyo wa Serikali alidai alikutana na Muro kwenye mgahawa wa California na mawasiliano yao yalikuwa yakifanyika kwa simu ya mkononi na upande wa Serikali katika kesi hiyo iliwasilisha mahakamani picha za CCTV, zikionesha watu watatu ambao walidaiwa kuwa ni washitakiwa.



Vile vile upande huo wa mashitaka ulidai kuwa Muro alimwandikia Wage ujumbe Januari 31 mwaka jana, akisema: “Vipi mbona hupatikani?” Mahakama iliona kuwa ushahidi huo ni dhaifu.



“Mahakama imeona kuwa mawasiliano ni jambo la msingi, kwa sababu ili kula njama ni lazima watu wawasiliane, na kutokuwapo nakala ya maandishi ya ujumbe huo ni upungufu mkubwa katika mashitaka hayo.



Hakimu Moshi alisema hakuna ushahidi katika mashitaka ya kula njama, kwani upande wa mashitaka ungeweza kuwasiliana na watu wa mtandao wa simu na kuleta nakala ya mawasiliano yao na dereva wa Wage aliyedaiwa kuwa na Wage katika mgahawa wa California ili athibitishe kama Wage na Muro walikutana. Pia Mahakama hiyo iliona kuwapo na kila sababu ya upande wa mashitaka kuleta DVD kuonesha mahakamani kupitia video.



“Hivyo mashitaka haya yanaacha wasiwasi mwingi na Mahakama inawaachia huru kwa mashitaka hayo washitakiwa wote,” alisema.



Katika mashitaka ya pili ya kuomba rushwa yakiwakabili washitakiwa wote, Mahakama iliangalia kama yalithibitishwa na upande wa mashitaka bila kuacha shaka, Hakimu Moshi alisema upande wa mashitaka ulikuwa na shahidi Wage na maelezo ya washitakiwa.



Alisema katika ushahidi wake, Wage alidai kuwa Muro akiwa na wenzake alimwambia kuwa watamsaidia kwenye tuhuma zinazomkabili akiwapa Sh milioni 10, lakini akawaeleza kuwa hakuwa nazo wakati huo ila alikuwa na Sh milioni moja na kuwapa.



“Mbali na ushahidi huo, hapana shaka kwamba hakuna ushahidi mwingine wa upande wa Serikali unaoonesha kuwa walipokea fedha hizo, Mahakama ilitazamia kuwapo ushahidi wa mawasiliano kama wa kuona haupo,” alisema Hakimu Moshi.



Akiendelea kusoma hukumu hiyo huku washitakiwa wakiwa wamesimama na kijasho kikiwatoka kwa wasiwasi, hasa pia kutokana na chumba cha Mahakama kuwa kidogo, kulinganisha na wasikilizaji wengi waliokuwapo, alisema upande wa mashitaka pia ulikuwa na uwezo wa kuwasilisha mahakamani nakala ya mawasiliano kutoka kampuni ya simu kuthibitisha.


Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, Muro alikamatwa ndani ya gari, lakini Mahakama ilishindwa kuelewa ni kwa nini ilifanyika haraka, na pia eneo la hoteli ya Sea Cliff ni sehemu ya watu wengi, lakini hata hivyo washitakiwa wengine hawakukamatwa eneo la tukio, bali baadaye na kuunganishwa na kesi.



Kwa mashitaka ya mwisho yalioyokuwa yakiwakabili Mgasa na Kapama ya kujitambulisha kuwa ni maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mahakama hiyo pia ilisema inawaachia huru washitakiwa kwa sababu hayakuthibitishwa.



Alisema kupitia ushahidi wa Wage, washitakiwa hao walipokutana naye walijitambulisha kwa majina ya Dokta na mwingine Musa, upande wa mashitaka ulitakiwa kufanya jitihada kufuatilia kama majina hayo wanayatumia mtaani, kwa sababu washitakiwa wenyewe walikana kuyajua.



Aidha, Hakimu katika hukumu hiyo alihoji Wage akiwa msomi aliwezaje kukubali mtu ajitambulishe kwa mdomo kama ofisa wa Takukuru bila kuoneshwa vitambulisho na akakubali?



“Mahakama imeangalia pia katika mashitaka haya na kuona kubakia shaka na upande wa mashitaka katika ushahidi wake, hakuna vielelezo na ushahidi wa kuthibitisha hilo bila kuacha shaka, hivyo katika mashitaka haya Mahakama inawaachia huru,” alisema Hakimu Moshi.


Hakimu alimalizia hukumu yake akisema stakabadhi, pingu na miwani havikubishaniwa katika kesi na kwa kuwa vilipatikana kwa stakabadhi, basi warudishiwe wahusika, hata hivyo, alitangaza kuwa upande usioridhika rufaa iko wazi.



Mwendesha Mashitaka wa kesi hiyo ambaye ni Wakili wa Serikali, Boniface Stanslaus alipotafutwa kwa simu kuhusu kesi hiyo alisema hajajua kama watakata rufaa ila anapeleka taarifa ya hukumu hiyo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ambaye ndiye ataamua.



Muro, mbali na kusema kuwa anasamehe waliomfitini, aliwaasa wanahabari kutokuwa waoga na waungane kukabiliana na changamoto na kuibua maovu. Aliondoka mahakamani hapo akiwapungia mkono waandishi wa habari akiwa kwenye gari dogo jeupe namba T 117 BAE saa 04.48 asubuhi ikiendeshwa na mkewe waliyefunga naye ndoa mwezi jana.



Muro, Kapama na Mgasa walipandishwa kizimbani Februari 5 mwaka jana na kusomewa mashitaka na Stanslaus akisaidiana na mwendesha mashitaka wa Ben Lincolin mbele ya Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe.


Washitakiwa hao baadaye waliachiwa kwa dhamana ya kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja na kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika na hivyo kuendelea kufika mahakamani wakati kesi ikiendelea.



Upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi saba na wa utetezi mashahidi wanne. Muro alidaiwa kujitambulisha pia kama kapteni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwatambulisha washitakiwa wenzake kuwa ni vigogo wa Takukuru.



Muro alidaiwa kuwa Juni mwaka jana alimpigia simu Wage akimtaka afike Dar es Salaam kwa kuwa ana tuhuma dhidi yake na alitaka kuzitoa kwenye kipindi chake cha Usiku wa Habari kupitia kituo cha televisheni cha TBC1 na alipofika wakamtaka atoe fedha hizo ili wasimtangaze.



Chanzo: Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment