Friday, November 25, 2011

Watuhumiwa CCM wagoma kujivua gamba

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete (kulia) akiteta jambo na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Nape Nnauye.


Mpango wa kujivua gamba ulioasisiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aprili mwaka huu unarejeshwa Kamati Kuu (CC) ambapo watuhumiwa wote wa makosa mbalimbali watafikishwa mbele ya Kamati za maadili na kuchukuliwa hatua kwa taratibu za chama hicho.


Mpango wa kujivua gamba ulilenga kuwashinikiza watuhumiwa wa ufisadi kuachia nafasi zao za uongozi ndani ya chama hicho na sasa unarejeshwa Kamati Kuu (CC) ili ichukue hatua zaidi kwa wale waliogoma kujiuzulu.


Hatua hiyo inatokana na kuwapo ukimya ambao unaashiria kutokuwapo viongozi na makada ambao wako tayari kujiuzulu nyadhifa zao kwa hiari yao kama ilivyotarajiwa.



Tangu kupitishwa kwa mpango huo maarufu kwa jina la kujivua gamba katika kikao cha NEC kilichopita cha Aprili mwaka huu, ni kada mmoja tu, Rostam Aziz aliyechukua hatua za kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Igunga na ujumbe wa NEC, lakini wengine wamekuwa kimya hadi sasa.


Katika kikao cha Aprili NEC hiyo ya CCM ilipitisha maazimio 26, lakini kubwa ni lile lililokuwa likihimiza vita dhidi ya ufisadi kuendelea na kutoa mwito kwa watu wanaotajwa na jamii kuhusika na ufisadi ambao wako ndani ya chama kujitathmini kisha kuchukua hatua za kuachia madaraka waliyonayo.Sehemu ya mwisho ya azimio hilo inasomeka:



“Wasipoachia madaraka chama kiwachukulie hatua mara moja”.Mmoja wa wajumbe wa CC ambaye ameomba jina lake kuhifadhiwa alisema:


“Tunawaomba NEC waturuhusu jambo hili tulifanyie kazi sisi (CC) na litafanyiwa kazi kupitia taratibu za kawaida za chama kwa kuzingatia kanuni na taratibu za maadili za chama hicho”.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment