Friday, November 25, 2011

Mapadri 3 waliokufa ajalini kuagwa Pugu

IBADA ya Misa ya kuwaaga mapadri watatu na mlei, raia wa Italia waliokufa katika ajali ya gari katika eneo la Ruvu kwa Zoka, Bagamoyo mkoani Pwani hivi karibuni, itafanyika Jumapili asubuhi katika Parokia ya Pugu, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Pamoja na Ibada hiyo, siku hiyo kutakuwa na mkesha kuamkia Jumatatu ambapo kutafanyika Ibada nyingine ya Misa itakayoadhimishwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Salutaris Libena na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Yuda Thadeus Ruwaichi.

Mkuu wa Shirika la Wafransisco Wakapuchini nchini, Padri Wolfgan Pisa amesema,alisema ujumbe wa mapadri wawili wa shirika hilo kutoka Italia unatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya kuhudhuria ibada hizo kabla ya kusafirisha miili kwenda Italia.

“Ibada itakayoongozwa na Kadinali Jumapili itaanza saa 4.30 asubuhi na tukimaliza msafara utaelekea Msimbazi ambako ni makao makuu ya shirika letu hapa nchini, huko tutakuwa na mkesha wa maombolezo na miili ya wenzetu mpaka asubuhi Jumatatu,” alisema Padri Pisa na kuongeza:

“Jumatatu asubuhi kutakuwa na Ibada nyingine ya Misa Msimbazi saa 4.30 asubuhi itakayoongozwa na Askofu Libena na Askofu Mkuu Ruwaichi”. Askofu Ruwaichi pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Padre Pisa amesema, miili hiyo itasafirishwa Jumatatu jioni kwenda Italia baada ya taratibu kukamilika na mapadri wawili wa shirika hilo nchini, watasafiri pamoja nao kuongoza ujumbe wao kwenye maziko.

Hata hivyo Padri Pisa alisema mmoja wa mapadri waliokufa katika ajali hiyo, Silverio Ghelli, aliyekuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Pugu na ambaye alitarajiwa kuzikwa nchini kutokana na kukaa kwa zaidi ya miaka 30, naye atasafirishwa baada ya ndugu zake kuomba akazikwe Italia.

Mapadri wengine waliokufa katika ajali hiyo ni Liciano Baffigi na Corrado Trivelli, waliokuja nchini kusalimia Waitaliano wenzao na mlei Andrea Ferri.


Walikufa katika ajali ya gari wakiwa safarini kutoka Kongwa Dodoma kuja Dar es Salaam baada ya gari walilokuwemo aina ya Toyota Land Cruiser namba T903 ACQ, mali ya Parokia ya Pugu, Dar es Salaam, kugongana uso kwa uso na lori.


Chanzo: Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment