WASHAMBULIAJI Gaudence Mwaikimba, John Bocco na Hussein Javu, wametemwa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kitakachoshiriki michuano ya Chalenji inayoanza leo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilieleza kuwa wachezaji nane wameenguliwa katika timu hiyo na sasa wamebaki 20 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za mashindano.
Wachezaji hao walioenguliwa katika timu hiyo inayonolewa na Charles Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ni Deo Munishi (Mtibwa Sugar), Paul Ngelema (Ruvu Shooting) na Salum Telela (Moro United).
Wengine kwa mujibu wa Wambura ni Jimmy Shogi (JKT Ruvu Stars), Mohamed Soud (Toto Africans) na Daniel Reuben (Coastal Union).
Wachezaji waliobaki na timu zao katika mabano ni Juma Kaseja (Simba), Shaabani Kado (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba), Ibrahim Mwaipopo (Azam) na Juma Nyoso (Simba).
Wengine ni Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Shaabani Nditi (Mtibwa Sugar), Nurdin Bakari (Yanga), Haruna Moshi (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Simba).
Wengine ni Said Maulid (Angola), Musa Mgosi (DC Motema Pembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC), Mrisho Ngassa (Azam), Ramadhan Chombo (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe), Mbwana Samata (TP Mazembe) na Rashid Yusuf (Coastal Union).
Kilimanjaro Stars itacheza mechi yake ya kwanza kesho Ijumaa dhidi ya Rwanda kwenye ufunguzi wa michuano hiyo.
Wakati huohuo, timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’ imechukua nafasi ya Namibia kwenye michuano ya Kombe la Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) inayoanza kutimua vumbi leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye alisema jana kuwa Namibia imeshindwa kuja kwenye michuano hiyo, kwa sababu wachezaji wake wengi bado wapo kwenye Ligi Kuu ya nchi hiyo inayoendelea.
Kwa mujibu wa Musonye, Msumbiji nayo iliomba kuja kushiriki michuano hiyo ili ichukue nafasi ya Namibia, lakini wao wakaipa nafasi Zimbabwe ambayo pia iliomba.
Zimbabwe sasa inaingia moja kwa moja Kundi A lenye timu za Tanzania, Rwanda na Djibouti. Nyingine ni Uganda, Burundi, Zanzibar na Somalia zinazounda kundi B, huku kundi C likiwa na timu za Sudan, Malawi, Kenya na Ethiopia.
Chanzo: Gazeti la HABARILEO
No comments:
Post a Comment