Friday, November 25, 2011

Mjamzito 'aliyechinjwa' na lori hajatambuliwa

MJAMZITO aliyekufa kwa kugongwa na lori la mafuta na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili jijini Dar es Salaam bado hajatambulika.


Mwanamke huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 hadi 40 alikufa papo hapo Jumatano saa 7 mchana alipogongwa na lori hilo wakati anavuka barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam.


Polisi wamemtaja mwingine aliyekufa katika ajali hiyo kuwa ni Venon Sebastian (35-38), mkazi wa Kinyerezi, Dar es Salaam.


ajali hiyo iliyosababishwa na mwendokasi wa lori la mafuta lililoacha njia, ilihusisha magari saba eneo la River Side, Ubungo.

Polisi wanamtafuta dereva wa lori hilo la Kampuni ya Dalbit, Denis Benwelth (36), mkazi wa Morogoro ambaye inadaiwa alitoroka baada ya ajali hiyo.

Lori hilo lililokuwa likitoka Ubungo kuelekea Buguruni likiwa katika mwendo kasi, liliacha njia wakati likikwepa daladala iliyokuwa ikitoka kituo cha basi.


Baada ya kacha njia, lori hilo liliyagonga magari manne na kuyakanyaga vibaya magari mengine matatu.

Watu wanne walijeruhiwa katika ajali hiyo akiwemo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Yahaya Makame, amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam.

Kwa mijibu wa Polisi, majeruhi wengine ni Musa Charles (35) aliyevunjika miguu, amelazwa Katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Prosper Mwakitalima (31) mkazi wa Changanyikeni na Abbas Julius (24).

No comments:

Post a Comment