Friday, November 25, 2011

Lowassa, Sumaye wacharuka NEC

MAWAZIRI Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, jana walishambulia kwa maneno makali wajumbe wawili wa Sekretarieti ya CCM kwamba wamekuwa wakikivuruga chama na kusababisha mgawanyiko uliopo.



Lowassa aliyejiuzulu Uwaziri Mkuu, kutokana na kashfa ya Richmond ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumzia suala hilo wakati wa mjadala wa hali ya siasa, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichomazika jana mjini Dodoma.



Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Lowassa alianza kubwaga moyo wake baada ya NEC kuridhia ombi la Kamati Kuu ya chama hicho (CC) kwamba suala la mageuzi ndani ya CCM maarufu kama kujivua gamba lirejeshwe katika kamati hiyo ili lifanyiwe kazi kwa taratibu za kawaida za kinidhamu baada ya wahusika kukataa kuachia nafasi zao.


Mwenyekiti kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama wakinitukana, hivi hatukujua kwamba kuna kamati hizo za maadili,”Lowassa alinukuliwa akihoji.



Lowassa alinukuliwa akiwataja Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara, John Chiligati kwamba wamekuwa wakitukana watu ovyo kwa fedha wanazopewa na CCM.



Kwa mujibu wa taarifa hizo, Lowassa alitumia dakika saba kumshambulia Nape kwamba amekuwa akifanya mambo nje ya utaratibu na kwamba mwenendo huo umekuwa ukikibomoa chama badala ya kukijenga.



Baada ya maneno ya Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Sumaye alisimama na kuhoji sababu za chama hicho kunyamazia ukiukwaji wa taratibu ambao umekuwa ukifanywa na watendaji hao.


Mwenyekiti huyu bwana (Lowassa) amesema kwamba amechafuliwa kwa miezi saba, sasa kama leo tunasema kwamba tunarudi kwenye utaratibu wa kamati za maadili, hao waliomchafua watafanywaje?”



Sumaye alinukuliwa akihoji. Hata hivyo, taarifa za ndani ya kikao hicho zilimnukuu Kikwete akisema kwamba viongozi hao watakuchukuliwa hatua za kinidhamu kama watakuwa wamefanya hivyo.



Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete aliwasihi wajumbe kuachana na suala hilo na badala yake kuchangia maeneo mengine ya taarifa hiyo ya hali ya siasa iliyowasilishwa na Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje ya CCM, January Makamba.



Kikwete alinukuliwa akihitimisha hoja hiyo kwa kusema kwamba:



Jamani hapa tunajenga chama, watu wanasubiri kusikia tukimaliza kikao chetu kwa ugomvi, naomba tumalize kwa amani na twendeni tukajenge chama chetu”.



Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment