Saturday, October 15, 2011

Zitto, Mkulo jino kwa jino

WAZIRI wa Fedha, Mustafa Mkulo na Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha, Kabwe Zitto, wameendelea kuvutana kuhusu uhai wa Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC).


Wakati Zitto akimtuhumu Mkulo kuhusika na tuhuma za ubadhirifu, zinazolikabili shirika hilo na kumtaka waziri huyo ama ajiuzulu mwenyewe au Rais Jakaya Kikwete amfukuze, Mkulo alikanusha tuhuma zote na kusisitiza kujiuzulu hakupo kichwani mwake.


Zitto katika madai yake, alitaka Mkulo ajiuzulu wadhifa wake kupisha uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu shirika hilo.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Zitto alisema kumekuwapo na malumbano kuhusu shirika hilo tangu mkutano wa nne wa Bunge na hoja kubwa ikiwa ni kuvunjwa kwa CHC.


Katika hoja hiyo, Serikali ilipendekeza shirika hilo livunjwe, lakini Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), ilipinga lisivunjwe.


Alisema kutokana na malumbano hayo, Bunge liliamuru shirika hilo lipewe uhai wa miaka mitatu na kuagiza uchunguzi wa namna bora ya kuendesha shughuli za shirika hilo ufanyike.


Lakini kwa mujibu wa madai ya Zitto, kwa bahati mbaya Wizara ya Fedha iliamua kumsimamisha Mkurugenzi wa CHC kwa makosa aliyodai ya majungu na kuzusha kwamba shirika hilo liliwahi kuwahonga wabunge ili walitetee.


“Waziri Mkulo alilitaarifu Bunge kuwa Bodi ya CHC iliomba ukaguzi maalumu kuhusu tuhuma za ubadhirifu ndani ya shirika hilo, niliitaka pia Serikali ichunguze tuhuma kwamba Kamati ya POAC ilihongwa na kuahidi kujiuzulu nyadhifa zangu zote ikithibitika,” alisema Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema).


Alidai katika uchunguzi wake aligundua kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alitaka kumhoji Mkulo juu ya tuhuma zinazomkabili ndani ya shirika hilo, ikiwemo kuagiza CHC kuuza kiwanja chake kwa mtu aliyechaguliwa na waziri huyo.


Alidai kuwa anao uthibitisho wa nyaraka zote ikiwamo barua yenye kumbukumbu namba TYC/A290/13/4 na kwamba waziri huyo alikataa kutoa ushirikiano.


Alidai waziri huyo pia alitengua uamuzi wake wa kuongeza muda wa miezi mitatu wa bodi ya shirika hilo ambao ungemalizika Desemba mwaka huu na badala yake, akaivunja bodi hiyo wakati akifahamu hana mamlaka ya kufanya hivyo. Kwa mujibu wa Zitto, mwenye mamlaka ya kuvunja bodi hiyo ni Rais ambaye ndiye aliyemteua Mwenyekiti wa Bodi.


Kutokana na tuhuma hizo, Zitto aliomba Takukuru iingilie kati na kuchunguza tuhuma zote zinazolikabili shirika hilo na Mkulo na wakati uchunguzi huo ukifanyika, Mkulo ajiuzulu wadhifa wake wa uwaziri au Rais Kikwete amsimamishe. Pia alipendekeza ripoti ya CAG ikitoka, ipelekwe kwa Spika wa Bunge badala ya Hazina ili ifanyiwe kazi bila kuingiliwa.


Lakini Mkulo alisema hawezi kuzungumzia kwa undani suala hilo na kukiri kuwa yaliyojitokeza bungeni kuhusu CHC ni mengi na akiwa Waziri wa Fedha anatarajiwa kuwasilisha taarifa kuhusu shirika hilo katika Bunge linalotarajiwa kuanza mkutano wake Novemba 8, mwaka huu.


Kuhusu uhai wa Bodi hiyo, alisema tayari ilishaisha muda wake tangu Juni mwaka huu na Rais anazo taarifa na kwa kuwa ni mtu mzito mwenye majukumu mengi, suala hilo liko mikononi mwake kulishughulikia wakati wowote atakavyoona inafaa na si kutokana na shinikizo la mtu ye yote.


Alifafanua pia kuhusu tuhuma zinazomlenga za uuzwaji wa kiwanja na kushindwa kutoa ushirikiano; kwamba si za kweli na hata suala la madai kuwa POAC inadaiwa kuhongwa na CHC si ya kweli. Mkulo alisema ukweli ni kwamba Mbunge wa Viti Maalumu, Anastazia Wambura (CCM), ndiye aliyeanzisha hoja ya kuwapo kwa wabunge wanaolazimisha kutokuvunjwa kwa CHC na kutaka ufafanuzi ambao Mkulo alisema wizara yake itachunguza.


“Hakukutajwa Zitto wala POAC siku hiyo wala kuhusishwa na hongo na hata taarifa rasmi za Bunge zinaonyesha hivyo, mimi naomba tu mumuulize huyo mbunge mbona yeye ndio mwenye wasiwasi na kufuatilia sana suala hili la CHC?


“Kwa nini asingesubiri kwanza ripoti yangu ndipo aibue haya yote, kuna nini hapa? Ikumbukwe kuwa hili shirika linaendeshwa na Serikali na si POAC,” alisema Mkulo.


Chanzo: HABARILEO

No comments:

Post a Comment