Saturday, October 15, 2011

Wanaoishi na VVU hawataki kuitwa waathirika


WATU wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini Tanzania, wamesema si busara kuendelea kuwaita waathirika kwa sababu jina hilo linawanyanyapaa.


Wanataka watambulike kama watu wanaoishi na VVU, kwa kuwa jina hilo linawafanya wajisikie wenye kuthaminiwa, kuheshimiwa na kupendwa na jamii inayowazunguka, na hivyo kuishi kwa furaha kama raia wengine nchini.


Walisema hayo wakati wa mkutano wao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, iliyovikutanisha vyama vyao mbalimbali, likiwemo Shirikisho la Vyama vya wanaoishi na VVU nchini (TANOPHA) Chama cha Wanawake wenye VVU (TNW+) na vinginevyo, juzi.


Mbali na hilo, wamewaomba Watanzania watambue mchango wao katika maendeleo ya nchi, kufuatia harakati zao za uhamasishaji wa vita dhidi ya Ukimwi, inayowaepusha vijana wengi na maambukizi ya VVU, na hivyo kulinda nguvu ya taifa inayotegemewa zaidi katika uzalishaji.


Mratibu wa taifa wa Ukimwi wa TNW+, Joan Chamungu na Ofisa Mipango wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya Ukimwi (UNAIDS) tawi la Tanzania, Emmanuel Mziray walisema kuwaita wanaoishi na VVU kuwa ni waathirika ni ishara ya kuwanyooshea vidole na kuwatenga kwa nia isiyo njema.


Naye Chamungu aliwataka wanaowaita majina yasiyofaa kujaribu kuvaa viatu vyao japo kwa hisia tu na kuona namna wanavyoumizwa na majina tofauti wanayopachikwa kutokana na kuishi na VVU.


Walisisitiza kwa nyakati tofauti kuwa, ingawa Ukimwi unavuma zaidi kwa kuua, unyanyapaa ndio unaokatiza maisha ya wengi wao, wakiwemo wenye virusi vichanga ambavyo havijafikia hatua ya kuwafanya waugue.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lediana Mng’ong’o ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM-Iringa) alisema serikali, wanaharakati wa masuala ya Ukimwi na jamii inapaswa kupewa shukurani kwa kupunguza unyanyapaa uliokuwepo katika miaka ya 90.

Chanzo: HABARILEO

No comments:

Post a Comment