CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), sasa kimekiri kumeguka.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema, limeibuka kundi la watu wenye nguvu ya pesa, wanaokisaliti chama kwa kuendesha propaganda za kupotosha dhana ya kujivua gamba.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema kundi hilo linamhujumu pia Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, lakini akasema, chama kimejipanga kuwashughulikia wanaounda kundi hilo.
Alipotakiwa kutaja hujuma za kundi hilo dhidi ya mwenyekiti wa CCM, Nape alisema "Ni nyingi, moja ni kusambaza hoja ya kutaka nafasi ya urais itenganishwe na ile ya mwenyekiti wa chama."
“Wanafanya hujuma nyingi kwa mwenyekiti, lakini mojawapo ni hiyo ya kutaka kutenganishwa kwa kofia hizo mbili,” alisema Nape ambaye alisisitiza kuwa watu hao walianza kwa kuasi imani ya chama na sasa wanaendesha kampeni ya watu kuasi uamuzi halali wa vikao vya CCM.
"Juhudi hizi zimekuwa zikifanywa na kikundi kidogo sana cha watu wachache ambao kwa namna moja au nyingine wameathiriwa na mageuzi haya tunayoyafanya. Tatizo kakundi kenyewe kana nguvu kiasi ya pesa ndio maana kelele zao zinaonekana kuwa kubwa lakini, zisizo na mashiko," alisema NapeAliongeza:
"Chama tunafahamu na kufuatilia kwa makini kila kinachoendelea, hakuna tusichokijua juu ya juhudi hizi na zingine nyingi, zikiwamo jitihada za kutaka kumhujumu hata Mwenyekiti mwenyewe (Rais Jakaya Kikwete). Nasistiza tunazifahamu."
Nape alisema kinachotokea Arusha hivi sasa kwa UVCCM ni sehemu ya mwendelezo ya usaliti kwa chama chake ambo alisema ulianzia Igunga wakati wa uchaguzi mdogo na kusisitiza kuwa wahusika wanajulikana na njama zao hizo zitashindwa.
Kauli ya Nape imekuja siku chache tangu Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Beno Malisa atoe kauli ya kukikosoa chama na Serikali yake akiwataka makada wa CCM kuacha kuingilia siasa za Chadema pia kuitaka Serikali itafute suluhu ya matatizo yanayokabili wananchi.
Malisa pia alitaka wote waliohusika na kuvunjwa kwa mkataba wa Dowans, wawajibike kutokana na kile alichokiita ni kulitia taifa hasara.
Lakini Nape jana alisema msimamo wa CCM katika suala la kuilipa Dowans uko wazi.“Msimamo upo wazi na kilichofanywa na Tanesco kwenda mahakamani ndio msimamo wa Serikali ambayo ni ya chama kilichopo madarakani,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment