Thursday, October 13, 2011

UVCCM yawaonya wanaoutaka urais 2015

JUMUIYA ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imewataka vigogo wa juu wa chama hicho wenye nia ya kuwania Urais mwaka 2015, kuacha mara moja kuzuia shughuli za jumuiya kwa malengo yao ya kufanikisha kuwania nafasi hiyo.


Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa, aliyewataka vigogo wa CCM wanaowania nafasi ya urais mwaka 2015 ndani ya chama hicho, kuacha mara moja kuzuia shughuli za jumuiya hiyo na kuuomba uongozi wa juu kuwashughulikia haraka.


Alikiomba chama hicho kisiwaonee aibu vigogo hao na kuwafukuza kwani wanakivuruga chama hicho kwa maslahi yao kwa kuwatumia vijana wa UVCCM, kwani rais alishapatikana na muda wake haujamalizika, hivyo wasubiri hadi kipindi cha uchaguzi ila kwa sasa wafanyakazi za kuwatumikia wananchi.


Malisa aliyesema hayo kwenye Viwanja vya Mtakatifu Thomas jijini Arusha wakati akizungumza na wananchi na wakereketwa wa chama hicho kwenye ziara ya uzinduzi wa mashina ya wakereketwa wa Umoja wa Vijana.


Pia aliwaonya wanaCCM hao akisema wanachangia kwa kiasi kikubwa kukivuruga chama na kuwataka wajiondoe wenyewe kabla ya umoja huo kutoa shinikizo la kuwaondoa.


Aliwataka vijana wa CCM wajipange vema kufuatilia na kuwashughulikia vigogo hao haraka ili wasikipoteze chama hicho kwa kuwa muda mwingi wamekuwa wakiutumia kukikosoa chama cha upinzani, Chadema na kusahau kutimiza wajibu wao sanjari na kuondoa tofauti zao.


Aliwataka vijana kutolala katika kufanya kazi ya siasa na kugombea nafasi za uongozi bila ya kuhofu ili kutoa mawazo chanya katika kusukuma gurudumu la maendeleo, badala ya kuwaachia wazee pekee kuwamulia.


Chanzo:HABARILEO

No comments:

Post a Comment