Thursday, October 13, 2011

Wafungwa wamponza askari Magereza

TUME ya Utumishi wa Jeshi la Polisi na Magereza nchini, imemshusha cheo askari Magereza kwa kosa la kuwaruhusu wafungwa wawasiliane na watu wa nje kwa simu.


Tume hiyo pia imeridhia kufukuzwa kazi kwa askari Polisi mmoja kwa kosa la kuomba rushwa na kutaka kumbambikizia raia kesi.


Mwingine kafukuzwa kazi kwa kumjeruhi raia kwa kukusudia na mwingine kwa kosa la kumwezesha mahabusu kutoroka.


Uamuzi huo ulitolewa juzi na Tume hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, mbali na hao, pia Tume hiyo imeridhia kufukuzwa kazi kwa askari Magereza wengine wawili kwa makosa ya utoro kazini.

Uamuzi wa Tume hiyo, unatokana na kukataliwa kwa rufaa zilizokuwa zimepelekwa mbele ya Tume hiyo na skari hao na umetolewa kwa kufuata Sheria namba 8 ya mwaka 1990.


“Tume hii itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria askari wote watakaobainika kukiuka maadili ya kazi zao,” alisema Waziri Nahodha katika kikao hicho.


Alisema askari watakaoshughulikiwa bila huruma ni pamoja na wale watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa, watakaobainika kuwabambikizia kesi raia na watakaobainika kuvuruga utaratibu wa kuwatunza wafungwa magerezani.


Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga alisema kwa taratibu za majeshi hayo, kwa sasa si vyema kuwataja wahusika kwa majina.
Chanzo: HABARILEO

No comments:

Post a Comment