Wednesday, June 29, 2011

Halima Mdee amuonya Mwenyekiti wa Bunge


Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, akifurahia jambo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.


MBUNGE wa Kawe (Chadema) Halima Mdee jana alimtolea uvivu Mwenyekiti wa Bunge, Sylivester Mabumba kwa kumweleza kuwa akiendesha mjadala kwa ushabiki kiti cha Spika kitamshinda.


Mvutano kati ya Mdee na Mabumba jana jioni ulisababishwa na kauli za Mbunge wa CCM, Zarina Madabida kusema wanaopinga posho za wabunge
(sitting allowance) wanataka chama chao kiwafidie fedha hizo.


Kauli ya Mbunge huyo ilisababisha Mdee asimame akaomba
mwongozo.


Madabida alikuwa akichangia hotuba ya bajeti ya ofisi za Waziri Mkuu ya mwaka 2011/12 jana na bila kukitaja chama hicho alisema kama kina dhamira ya kweli ya kukataa posho hizo kwanini wabunge wake wanataka kufidiwa
posho hizo na chama.


“Mwenyekiti hizi posho ni muhimu, mimi leo nikienda Dar es Salaam akinamama nakwenda kuwasaidia na hizi posho,” alisema Madabida.


Baada ya Madabida kumaliza kuchangia hotuba hiyo na kukaa chini, Mdee aliomba mwongozo wa mwenyekiti huku akitaja kanuni ya bunge inayomtaka Mbunge asiseme uongo na endapo atasema jambo hilo atatakiwa alithibitishe.


Lakini kabla hajamaliza kukifafanua kifungu hicho, Mabumba alimtaka Mdee akae chini, lakini Mbunge huyo kabla ya kukaa alisita kwa sekunde kadhaa halafu akakaa.


Mabumba alimweleza Mdee kwamba, Madabida wakati akizungumza hakutaja chama chochote na endapo angekitaja chama hicho ndio angetakiwa kuthibitisha.


Baada ya ufafanuzi huo, Mdee alinyanyuka na kusema kwamba chama kinachopinga posho ni Chadema na NCCR-Mageuzi.

“Kwa implication, Mheshimiwa Madabida alikuwa anavilenga vyama hivi… Mwenyekiti usikikalie kiti kwa ushabiki, kitakushinda,” alisema Mdee.


Hata hivyo kabla hajaketi, ilisikika sauti ndani ya bunge ikisema “Jumamosi mligombea posho’’ hatua iliyomfanya Mdee kumtaka mwenyekiti huyo wa Bunge amlinde.

No comments:

Post a Comment