Wednesday, June 29, 2011

Mbunge- Kuna mambo ya kihuni serikalini

Spika wa Bunge, Anne Makinda, akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.



Mbunge wa Kasulu Mjini mkoani Kigoma, Moses Machali jana alivutana na Spika wa Bunge, Anne Makinda, baada ya Mbunge huyo kusema bungeni kuwa, ndani ya Serikali kuna mambo ya KIHUNI yanafanyika.


Kwa mujibu wa Mbunge huyo, mwaka uliopita zilitengwa zaidi ya Sh6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kidawe-Kasulu kwa kiwango cha lami lakini, fedha hizo hazijawahi kutolewa na kwamba hata katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi 2011/12 fedha hizo hazijatengwa.


“Kuendelea kuwaahidi wananchi wakati jambo lenyewe halijafanyika ni uhuni wa serikali.., inawafanyia uhuni watu wa Kigoma,”alisema Machali.

Kauli hiyo ilisababisha Makinda amuamuru Mbunge huyo atumie lugha nzuri anapochangia na aache kutumia neno ‘uhuni’.


“Barabara inaanza kujengewa Nyakanazi.., Nyakanazi sio Kigoma. Hivi Kigoma tumewakosea nini, Rais Kikwete alisema barabara itajengwa, lakini leo mmezihamisha fedha hizo sehemu nyingine, kama sio uhuni ni nini,”aling'aka Machali.


Kitendo cha Machali kurudia neno hilo kilisababisha Makinda amuonye tena Mbunge huyo na kumweleza kuwa akitumia neno ‘uhuni’ anaweza asisikilizwe na anaowapelekea ujumbe huo.


Mbunge huyo alionekana kutokubaliana na Spika kwa kujibu kuwa “Hata Shelukindo alitumia neno ‘kijingajinga’ na alikuwa akitulenga sisi wapinzani, sasa sisi wapinzani tukitumia maneno ya ukali tutahukumiwa, spika tuwe na 'check and balance' (kuangalia usawa)”.


Machali alikuwa akinukuu mchango wa Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo (CCM), ambaye wakati akichangia bungeni alisema kumekuwa na wabunge wanaoingiza hoja za kijingajinga bungeni.


Machali aliweka wazi kwamba wabunge ni kama wamejivua uwakilishi wa wananchi kwa kuwa, wamekuwa mbogo dhidi ya hoja ya kufutwa kwa posho za vikao.


Alisema, maendeleo ya Tanzania hayalingani na umri wa miaka 50 ya Uhuru wake na kwamba, wananchi wa Tanzania hawana amani, bali wana utulivu ulioambatana na nidhamu ya woga.


“Siwezi kukubali kuwa kuna amani, wakati watu wanawaza watapata wapi mlo, polisi wanaendeleza vitendo vya kuwapiga raia kama wakimbizi ndani ya nchi yao, Serikali inakaa kimya na kusema mamlaka husika ziachwe zifanye kazi yake,”alisema.

No comments:

Post a Comment