Wednesday, June 29, 2011

Moto wa waua mume, mke, watoto 2

WATU wanne wa familia moja wakiwemo baba na mama wa familia wamekufa kwa kuungua moto ndani ya nyumba walimokuwa wamelala mkoani Tabora.


Nyumba hiyo iliteketea kwa moto Jumatatu, saa mbili usiku katika kijiji cha Ipululu, kata ya Igalula, wilayani Uyui.


Diwani wa kata ya Igalula, Said Kapalu amesema moto huo uliolipuka ghafla ulienea kwa haraka na kusababisha vifo vya mke na mume papo hapo.


Amesema, watoto wao wawili wa wanandoa hao walifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya mkoa wa Tabora, Kitete.

Amewataja walioaga dunia kuwa ni baba wa familia hiyo, Sango Abel na mke wake, Neema Hamad pamoja na watoto Mariam Sango na Twabi Sango.

Kwa mujibu wa diwani huyo, chanzo cha moto huo ni kulipuka kwa dumu lililokuwa limehifadhi mafuta aina ya petroli.


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.


Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Dk Masudi Lifoba, alisema watu hao walikufa kutokana na majeraha makubwa ya moto.


Diwani Kapalu amesema, baada ya mafuta hayo kulipuka na nyumba kuanza kuwaka moto, watoto hao walifanikiwa kujiokoa kwa kutoka ndani ya nyumba hiyo, lakini nguo walizokuwa wamevaa ziliendelea kuwaka.


Alisema, wasamaria wema walijitahidi kuwaokoa kwa kuzima moto uliokuwa umeshika mavazi yao, lakini tayari walikuwa na majeraha makubwa kutokana na kuungua vibaya katika sehemu mbalimbali za miili yao.


“Baada ya kuzima moto uliokuwa unawaka kwa kasi kwenye miili ya watoto, ilibidi wawakimbize haraka kwenda hospitali ya Kitete lakini kwa bahati mbaya, baadae walifariki,”alisema Kapalu.


Alisema wananchi kwa ushirikiano waliweza kuudhibiti moto uliokuwa ukiwaka na kuweza kuiokoa nyumba isiungue ingawa mali mbalimbali ziliteketea kabisa kwa moto.


Baadhi ya wakazi wa kata ya Igalula hujishughulisha na biashara isiyo rasmi ya kuuza petroli, ambapo huifadhi mafuta hayo ndani ya nyumba zao hivyo kuhatarisha maisha yao.


Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walisema familia iliyoteketea kwa moto ilikuwa miongoni mwa nyingine za kijiji hicho ambazo hujihusisha na biashara ya aina hiyo.


Walidai si rahisi kwa familia nyingi kijijini hapo kuacha biashara hiyo kwa sababu ndiyo wanayoitegemea kupata kipato.

No comments:

Post a Comment