Saturday, October 24, 2009

Mume amuua mke kwa kisu

POLISI mkoani Rukwa inamshikilia mkazi wa hapa, Anthony Tundu (30) kwa tuhuma za kumuua kwa kumchoma kisu mkewe, kisha naye kujichoma kisu kwa nia ya kujiua kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isunto Mantage, amesema,tukio hilo lilitokea Oktoba 22 mwaka huu saa 6.45 usiku, baada ya wanandoa hao kurejea nyumbani wakitoka katika kilabu cha pombe.

Inadaiwa kuwa,baada ya kuingia chumbani ulizuka mzozo baina yao, Tundu alimtuhumu mkewe, Sabina Sasala (25), kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na baadhi ya vijana katika eneo hilo.

Inadaiwa kuwa,Tundu,alimweleza mkewe kuwa, hali hiyo inamvunjia heshima na kusababisha ndoa yao idharaulike.

Kamanda amesema,baada ya kuzozana kwa muda mrefu, wanandoa hao walipigana.

Wapangaji wenzao hawakwenda kuamua ugomvi huo kwa kwa madai kuwa,walikuwa wamechoka kuwasuluhisha, kwa sababu wanandoa hao wana na tabia ya kupigana kila wanapolewa.

Mantage amesema,baada ya kupigana kwa muda mrefu,Tundu alisikika akitoka nje huku akitukana na kuelekea jikoni.

Kamanda Mantage amesema, Tundu alichukua kisu,alikwenda nacho chumbani na kumchoma mkewe tumboni,
utumbo ukatoka nje na akavuja damu nyingi.

Kamanda amesema,mwanamke alilia kwa sauti kubwa akiomba msaada kwa majirani, walifika chumbani na kumkuta sakafuni,mumewe alikwishakimbia.

Majirani walimchukua na kumkimbiza kituo cha Polisi cha mjini hapa, wakampeleka katika Hospitali ya mkoa mjini Sumbawanga akiwa amepoteza fahamu,akafariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, majirani walimtafuta Tundu, wakamkuta kichakani akiwa na jeraha kubwa tumboni, kisu kilikuwa pembeni yake,alikitumia kujichoma, walimpeleka hospitali, amelazwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

No comments:

Post a Comment