Tuesday, July 28, 2009

Mwakyembe ajitoa mhanga

Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ameitaka Serikali iufunge mara moja mgodi wa dhahabu wa North Mara ili sumu inayodaiwa kutoka hapo isiendelee kuwadhuru wananchi.

Mbunge huyo pia ametaka mgodi wa dhahabu wa Geita ufungwe kwa sababu, kwa muda mrefu umekuwa ukitoa kemikali za sumu zinazowadhuru wananchi wa kijiji cha Nyakabale.

“Kwa nini tuogope wawekezaji kama mama mkwe?” amehoji Mwakyembe na pia kuuuliza kwa nini vifungu vya mikataba havitumiki kuwabana wawekezaji.

Kwa muda mrefu kumekuwa na madai kuwa mgodi wa North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara umekuwa ikimwaga maji yenye sumu katika mto Tigithe.

Kwa mujibu wa madai hayo, wananchi 21 kati waliyotumia maji hayo wamefariki dunia, wengine wamekumbwa na matatizo ya kiafya, na pia mifugo 200 imepoteza maisha.

Kampuni inayomiliki mgodi huo imekanusha taarifa hizo kwa madai kuwa polisi kwa kushirikiana na mamlaka za Wilaya ya Tarime zimefanya uchunguzi na kubaini kuwa hakuna uthibitisho wa kuwapo kwa madhara hayo.

Dk Mwakyembe amesema, anafahamu kwamba, kampuni inayomiliki mgodi wa North Mara, Barrick Tanzania, ni kubwa zaidi kwa uzalishaji wa dhahabu duniani na ina nguvu kubwa na inaweza kukutesa lakini hawezi kukaa kimya wakati wananchi wanaathirika na lazima hatua zichukuliwe.

“Hii nchi ni yetu, tutaongea kwa ujasiri tu” Dk Mwakyembe amesema bungeni mjini Dodoma wakati anachangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2009/2010.

No comments:

Post a Comment