MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania imesema aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, na aliyekuwa Afisa utawala wa ubalozi huo, Grace Martin, wana kesi ya kujibu.
Balozi huyo na afisa wake pia wanatuhumiwa kuhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh2 bilioni.
Uamuzi huo ulitangazwa jana asubuhi na Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Sivangilwa Mwangesi, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani ili itolewe uamuazi.
Akitoa uamuzi huo, hakimu Mwangesi alisema amepitia maelezo ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na vielelezo tisa vilivyotolewa ili kuthibitisha makosa dhidi ya watuhumiwa hao na kushawishika kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu.
Kwa mujibu wa hakimu huyo, watuhumiwa wanatakiwa kuanza kujitetea Mei 4, mwaka huu na kuwataka washtakiwa hao kupitia mawakili wao kueleza njia watakayotumia katika kujitetea na wataje idadi ya mashahidi wao.
Akijibu hoja hiyo, wakili Bob Makani anayemtetea Balozi Mahalu alidai kuwa mteja wake atajitetea yeye mwenyewe kwa njia ya kiapo na kwamba mashahidi wataitwa katika utetezi utakavyokuwa unaendelea.
Kwa upande wake, wakili Malima anayemtetea Martin, alidai mteja wake ataanza kujitetea yeye mwenyewe kwa njia ya kiapo na kwamba wataita mashahidi watatu.
Mara ya mwisho, ushahidi kuhusu kesi hiyo, ulichukuliwa katika ukumbi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam ambako mahakama ilikuwa inamsikiliza shahidi mmoja akiwa Roma Italia.
Shahidi huyo aliyewahi kutoa ushahidi wake Machi 14, mwaka jana alidai kuwa yeye alipokea mkataba wa mauzo wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia wa Euro 1, 032, 913.80 ambao unatambulika kisheria nchini humo.
Alidai sheria ya Italia inaruhusu mkataba mmoja wa wazi kama ule mauzo aliosaini yeye.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Septemba 23 mwaka 2002 huko Roma Italia, Mahalu na Grace Martin wakiwa waajiriwa wa Serikali ya ya Tanzania, walisaini hati ya malipo yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro 3,098,741.58.
Inadaiwa kuwa maelezo hayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao.
No comments:
Post a Comment