Tuesday, February 3, 2009

Kifo cha magazeti?


Habari za leo wadau, bado nipo chuoni IFM Dar es Salaam katika kituo TGDLC napata nondo kuhusu masuala ya uandishi wa habari katika dunia ya leo ya utandawazi.

Nipo na wadau wa taaluma hii wakiwamo waandishi wa habari waandamizi, wahariri wa habari, na watangazaji wa radio na televisheni hapa Tanzania.

Kwa ujumla mafunzo ni mazuri, tumepanua ufahamu wetu kuhusu mambo mengi yanayohusiana na majukumu yetu, na tumepewa pia changamoto za kutuwezesha kufikiri kuwa itakuwaje miaka ijayo.

Moja ya mambo tuliyojifunza leo ni kuhusu taaluma ya uandishi wa habari katika dunia ya sasa iliyotawaliwa na matumizi ya intaneti kama moja ya njia kuu za mawasiliano.

Kwa ujumla intaneti imebadili mfumo wa maisha ya mtu mmoja mmoja na pia kuathiri namna wanadamu wanavyowasiliana kupitia vyombo vya habari.

Miaka ya nyuma magazeti yalikuwa ni moja ya njia kuu za kupashana habari lakini kadiri miaka inayosonga mbele hali inabadilika, watu wengi hasa mijini wanapata habari kwenye mtandao kuliko kusoma magazeti hivyo kuathiri pia mauzo ya magazeti na machapisho mengine kwa ujumla.

Takwimu zinaonyesha kwamba, matumizi ya intaneti barani Afrika ni madogo kulinganisha na mabara mengine, China inaongoza kwa wingi wa idadi ya watu wanaotumia mtandao wa intaneti kuwasiliana.

Ingawa ni takribani asilimia nne tu ya Watanzania wanatumia intaneti, kazi ya matumizi imekuwa ikiongezeka kwa kuwa mabadiliko ya Teknolojia ya Tabari na mawasiliano (Teknohama) yamerahisisha si tu namna ya kuwasiliana bali pia upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano.

Nina mashaka na hali ya baadaye ya biashara ya magazeti kwa kuwa hivi sasa si lazima ununue gazeti kwa kuwa habari zilizomo humo zinapatikana kwenye intaneti.

Kwa kuwa hapa nchini sehemu kubwa ya magazeti yanauzwa mijini, na kwa kuwa watumiaji wa intaneti wapo kwenye maeneo hayo, endapo kasi ya matumizi ya mtandao itafikia ile ya Ulaya na Asia, kutakuwa na haja gani ya kununua gazeti?

Mliowekeza kwenye biashara ya kuchapisha magazeti lifikirieni hilo kabla hali haijawa mbaya.

Wenye maduka ya kuuza seti za televisheni kaeni chonjo kwa kuwa kama huduma ninayoipata kwenye chombo hicho, mfano kuangalia miziki, kutazama habari nk naweza kuipata kwenye simu au Laptops kuna haja gani ya kununua TV Screen kuuubwa.
------------------------

No comments:

Post a Comment