Wednesday, August 29, 2012

Askofu alianguka bafuni, waumini wazimia kanisani

Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda, Padre Patrick Kasomo amewaeleza waumini katika kanisa kuu la Jimbo la Mpanda kuwa, Askofu Paschal Kokiti (55) alipatwa na shinikizo la damu Jumapili asubuhi Agosti 27,2012 akakutwa hana fahamu.
 
Aliwaeleza waumini hao kuwa Askofu Kikoti alipatwa na ugonjwa huo saa moja asubuhi moja asubuhi wakati akioga, akaanguka akiwa bafuni akapoteza fahamu.
 
Kwa mujibu wa Padre Kasomo, mapadre na masista walibaini kuwepo kwa tatizo hilo walipotoka kwenye ibada ya misa ya kwanza  saa mbili na nusu.
 
Amesema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilitafuta ndege siku hiyo hiyo,ikaenda kumchukua Askofu Kikoti jimboni Mpanda na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza.
 
Padre Kasomo amesema, Askofu Kikoti aliaga dunia jana saa 2:30 usiku.
 
Baada Padre Kasomo kutoa taarifa hiyo waumini wa kanisa hilo walianza kulia na baadhi yao walipoteza fahamu.
 
Marehemu Askofu Paschal Kikoti alizaliwa Mkoani Iringa katika Parokia ya Nyabula mwaka 1957 , alipewa daraja la upadre tarehe 29/6/1988 mkoani humo.
 
Alipewa daraja la uaskofu 14/01/2001 na kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Mpanda.
 
Mwili wa Askofu Kikoti unatarajiwa kuzikwa Jumamosi wiki hii ndani ya Kanisa Kuu la Mpanda.

No comments:

Post a Comment