Wednesday, May 30, 2012

Waziri Nchimbi, Polisi wazijadili vurugu Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania Dk.Emmanuel Nchimbi, akizungumza na Viongozi wa Jumuiya za Kiislamu na Wadau wa Sekta ya Utalii Zanzibar, kuhusiana na fujo zilizotokea Zanzibar, Kulia Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Said Mwema na (kushoto) Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali.

Waziri Dk. Nchimbi  akisisitiza jambo katika Mkutano wake na Viongozi wa Dini  kuzungumzia Vurugu zilizotokea katika mitaa ya mji wa Zanzibar.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Said Mwema, akizungumza katika Mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar Kilimani

WAKATI Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ikikiri kuwepo kwa watu wanaotumia mgongo wa dini kutimiza malengo yao ya kisiasa, hali ya hatari imezidi kugubika mji wa Zanzibar, baada ya watu wasiojulikana, lakini wakiaminika kuwa wafuasi wa kundi la kidini la Uamsho kuyashambulia na kuteketeza makanisa sita hadi kufikia jana.

Kadhalika, shule nyingi za msingi na sekondari, tangu juzi zimefungwa, baadhi yake zikiwemo za bweni, huku kukiwa na habari kuwa wanafunzi katika shule mbili walilazimishwa kurejea makwao hadi hapo hali ya utulivu itakaporejea.
Mmoja wa wakuu wa shule hizo, ambaye aliomba jina lake na shule vihifadhiwe, alikiri kuwa shule yake imesimamisha masomo kwa muda usiojulikana, na kwamba wamewaruhusu wanafunzi wanaoshi bwenini kurejea makwao.

Uchunguzi umebaini kuwa, karibu shule zote za msingi na sekondari zinazomilikiwa na serikali na taasisi za dini, zilizoko Mjini Magharibi, tangu juzi hazijafunguliwa, na wanafunzi wachache waliopata ujasiri wa kufika shuleni, walirudishwa majumbani na walimu.
Hadi kufikia jana, makanisa yaliyothibitika kuchomwa moto na watu hao wanaoaminika kuwa wafuasi wa kikundi hicho cha Uamsho ni Kanisa la EAGT, Elimu Pentekoste, TAG, Anglikana, Katoliki na FPCT.

Askofu wa Jimbo la Zanzibar wa Makanisa ya Tanzania Assemblies of God (TAG), Dickson Kagenga aliilaumu serikali akisema imechelewa kuchukua hatua kukomesha vitendo vya uchomaji moto makanisa mara tu vilipoanza.

Askofu Kagenga alisema, uchomaji moto wa makanisa hayo, usingefikia hatua hii mbaya, kama vyombo vya dola vingewakamata na kuwashughulikia kisheria wahusika, lakini hapakuwa na hatua iliyochukuliwa, hivyo kuwapa mwanya na jeuri watu hao kufanya wapendavyo.
Hivyo, ameiomba serikali ichukue hatua za kisheria kwa wahusika wote kwani matokeo hayo yanahatarisha maisha ya watu.

Akizungumzia suala hilo mbele ya waandishi wa habari jana, Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, pamoja na kulaani mashambulizi hayo, alisikitishwa na ukimya wa serikali wa muda mrefu juu ya vitendo vya uchochezi na uvunjifu wa amani uliokuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi wa makundi ya kiislamu dhidi ya watu wa dini nyingine.

Alisema katika siku za hivi karibuni kumeibuka makundi ya kidini yaliyoanza kutoa matamko yenye kuchochea ghasia za kidini, na kulitaja kundi la JUAKATA lililowahi kufanya kongamano katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam, kama moja ya makundi ambayo kauli zake zinahatarisha amani.

Mtokambali alidai kuwa, katika kongamano hilo, badala ya kujadili mambo ya dini na kudumisha amani, walihamasisha washiriki kuhakikisha kuwa rais ajaye lazima atoke Zanzibar.

Aliongeza kuwa, mambo mengine yalikuwa haja ya kukabiliana na ukuaji wa wakazi wa Kikristo, kupinga muungano ili kuupa nguvu Uislamu na kupigana kufa na kupona kutetea maslahi yao katika kipindi cha kuandaa katiba.

Askofu huyo alisema ameingiwa hofu kwa kuwa roho ya ubaguzi wa kidini ambayo ilikemewa na Hayati Mwalimu Nyerere na kuifananisha na dhambi ya kula nyama ya mtu imekua ikiyatafuna mataifa ya Afrika.

Alisema taswira hiyo ni mbaya, na kama haitapatiwa dawa italigawa taifa na kulifanya kama ilivyokuwa kwa Nigeria na kwingineko barani Afrika.

Hata hivyo, alitoa ushauri kwa serikali na viongozi wa dini kukumbuka kuwa wana wajibu mkubwa katika jamii, hivyo ni vema wakawa makini katika kutoa matamshi na maelekezo yao ili yasiwe chanzo cha kuchochea vurugu za kidini na uvunjaji wa amani.

Mtokambali alisema ni vyema kwa wakati huu wa kuandikwa kwa katiba mpya kila kikundi kikafuata utaratibu uliowekwa badala ya kuchochea kwani madhara yake yatawakumba Watanzania wote ikiwa ni pamoja na watoto.

“Ni vyema ieleweke kuwa matukio kama haya ya uvunjaji wa amani yasipodhibitiwa na kukomeshwa haraka, yanaweza kuumba chuki ambayo inaweza kuibua mlipuko mkubwa na machungu kwa wananchi na matokeo yake yakawa mabaya kwa taifa zima,” alisema.


Waziri katika ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammd Aboud amekiri kuwa vurugu hizo zina mkono wa siasa ndani yake, na kwamba serikali ilikosea kudhani kuwa wahusika ni viongozi wa dini.

Akiwa katika ziara yake kukagua uharibifu uliofanywa katika Kanisa la Kariakoo, Waziri Aboud alisema serikali imekosea kuwaachia watu ambao wametumia kivuli cha dini kutekeleza matakwa yao ya kisiasa wakati taasisi zao zimesajiliwa rasmi kidini.

Kutokana na kubainika kwa jambo hilo, serikali imeamua kuendesha msako mkali kuwakamata watu wote watakaohubiri maneno yatakayohamasisha vurugu.

Alisema serikali iko wazi kusikiliza maoni ya mwananchi yeyote yatakayofuata utaratibu, sheria na kanuni za nchi kwa nia ya kujenga Zanzibar mpya inayokabiliwa na matatizo ya kiuchumi, ajira na kupambana na umaskini unaohitaji umoja, mshikamao na utulivu ili kuyashinda.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali, Saidi Mwema alisema watawakamata na kuwafikisha mahakamani watakaohusika na vurugu hizo na kwamba jeshi lake limejipanga kukabiliana na vurugu.

Habari-Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment