Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema, waraka uliosambazwa kumchafua mgombea wa ubunge Arumeru Mashariki kwa tiketi ya chama hicho, Sioi Sumari hauna uhusiano wowote na CCM na hakuna Mbunge wala mwanachama wa chama hicho tawala anayeweza kufanya hivyo.
“Hizi ni kampeni za kipuuzi kabisa na sijui kwa nini tunafika huko. Nakuhakikishia waraka huo hauna uhusiano kabisa na CCM, kwanza hatujauona na hauwezi kuandaliwa na mwanachama yeyote wa CCM,” alisema Nape.
Nape aliituhumu CHADEMA kwamba inahusika na waraka huo na kwamba ndio waliouandaa kwa lengo la kumchafua mgombea wao.
“Huo ni waraka wa CHADEMA na najua wamefanya hivi kulipiza kisasi kwani wao waliwahi kufanyiwa hivyo Igunga na Arumeru na watu wao wa CHADEMA, wakafikiri ni CCM, hivyo naona wanalipiza kisasi,” alisema Nape na kuwataka wana CCM waupuuze na watambue kuwa Sioi ndiye chaguo la CCM.
Kwa upande wao CHADEMA, Mkuu wa Operesheni na Uchaguzi wa CHADEMA, John Mrema, alikana chama chake kuhusika na waraka huo akifafanua kuwa hizo ni siasa za kijinga ambazo CHADEMA kama chama makini kinachoheshimika, hakiwezi kuzifanya.
“Hizi ni siasa za kijinga ambazo kamwe CHADEMA kwa heshima iliyonayo, hakiwezi kuzishiriki kwani tumejipanga kunadi sera ili mgombea wetu Joshua Nassari apate ushindi wa kishindo,” alisema Mrema.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa huenda waraka huo umeandaliwa na makundi yanayokinzana ndani CCM yanayotokana na majeraha ya kura za maoni na harakati za urais mwaka 2015.
Huu ni waraka wa tatu kusambazwa kwenye jimbo hilo tangu kuanza kwa kampeni.
Waraka wa kwanza ulidaiwa kuandaliwa na Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ukiwalaumu viongozi wa CHADEMA akiwemo meneja kampeni wa chama hicho, Vicent Nyerere, kwa madai ya kumshambulia Rais mstaafu Benjamini Mkapa kwa kumhusisha na kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Waraka mwingine uliandaliwa hivi karibuni na watu wasiojulikana dhidi ya Dk. Slaa ambao unaungana na waraka uliodaiwa kuwa ni wa Zitto kubeza viongozi wa chama hicho wanaomchafua Mkapa.
Katika hatua nyingine, taarifa zinasema kuwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, pamoja na Nape, wanatarajia kupanda jukwaani keshokutwa kumnadi mgombea wao.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao wa CCM kukaa na kupanda jukwaa moja tangu mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete alipoasisi vita ya kujivua gamba, huku Nape akimtaja hadharani Lowassa kama mmoja wa wanachama wa CCM wanaopaswa kujivua gamba.
Hali hiyo imewafanya wanasiasa hao kuonekana kama mahasimu kisiasa na ni nadra kwao kukutana au kufanya shughuli za chama pamoja.
Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli, anapanda jukwaani kumnadi Sioi ambaye pia ni mkwewe, huku Nape akilazimika kufanya hivyo kuhakikisha CCM inaibuka mshindi.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment