Tuesday, December 6, 2011

Polisi wadaiwa kutishia kumlawiti mtuhumiwa

Mshitakiwa Ayub Yusufu (26) amedai mahakamani kuwa, alitishiwa kulawitiwa na askari sita ili akiri kumshambulia askari wa usalama barabarani, Abihud Kasonde.


Mshitakiwa huyo alidai mbele ya Hakimu Ferdinand Njau katika Mahakama ya Mwanzo Utemini mjini Singida kuwa, alitiwa mbaroni na Polisi Ijumaa iliyopita alipokuwa mahakamani hapo kusubiri kumdhamini mwenzake.


Amedai kuwa, baada ya polisi kumkamata walimuunganisha katika kesi hiyo.


Alidai kuwa alifika mahakamani ili kumwekea dhamana mmoja wa wafanyabiashara wa kuku, lakini alikamatwa na askari waliokuwepo mahakamani hapo wakiongozwa na mlalamikaji, Abihud.


Yusufu alidai kuwa baada ya kukamatwa, aliingizwa katika gari la polisi lililokuwa limeegeshwa mahakamani na kupelekwa nje kidogo ya mji, eneo la Ziwa Kindai ambako alipigwa na kutishiwa kuwa lazima wamlawiti.


“Walinivua shati na viatu na kunipiga miguunihuku wakinilazimisha nivue suruali. Nikakataa hadi ikachanika lakini sikuivua, nikasema niueni tu….wakasema leo lazima tukulawiti….(kicheko mahakamani), baadaye wakanipeleka Kituo cha Polisi,” alidai Yusufu.


Alidai kuwa miongoni mwa waliomfanyia kisa hicho walikuwemo askari wawili wa kike na wanaume wanne, lakini walioshiriki ni askari wa kike mmoja na wengine wanaume.


Katika shauri hilo, mlalamikaji askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Konstebo Abihud anadai kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kuibiwa simu ya mkononi.


Anadai kufanyiwa vitendo hivyo baada ya kukamata lori lililobeba matenga yenye kuku waliokuwa wakisafirishwa na wafanyabiashara hao kwenda jijini Dar es Salaam.


PC Abihud alidai kuwa alilisimamisha lori hilo baada ya kuombwa na mgambo na watumishi wa Manispaa kwa kile walichodai wafanyabiashara hao walikwepa kulipa ushuru.


Washitakiwa wote walikana mashitaka na wapo nje kwa dhamana hadi Jumanne ijayo.


Chanzo: Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment