Monday, December 19, 2011

Kafulila- Nisameheni jamani, nitakwenda wapi?

Kilio cha kwikwi kilimtoka David Kafulila kuanzia saa 4:48, usiku baada ya mkutano kumvua uanachama.


Mwananchi lilifanikiwa kujipenyeza hadi ndani ya geti la ukumbi na kumkuta Kafulila akilia kwa sauti huku akiwa amepiga magoti na kumshika mmoja wa wajumbe miguuni.


‘’Nisameheni jamani..., naomba mnisamehe jamani nimekosa nitakwenda wapi?,’’ alisikika akilia.


Mbunge huyo alionekana kushindwa kujizuia na kuangua kilio kilicholeta huzuni kwa baadhi ya wajumbe wa mkutano huo ambao baadhi yao walionekana kumwonea huruma


Kutokana na hali hiyo, Mbatia alijaribu kumwombea msamaha kwa wajumbe, lakini walishikilia msimamo wao kwa maelezo kwamba kama Kafulila akisamehewa, wao watarudisha kadi za chama.


Katika wakati fulani Kafulila aliyekuwa amevaa suti nyeusi alikuwa alisimama nje ya mlango wa kuingilia katika ukumbi huo huku akiwa amekunja mikono yake, mfano wa mtu anayemwomba Mwenyezi Mungu


Wajumbe waliokuwa wakitoka katika ukumbi huo walionekana kutomjali na walimpita na kuingia katika magari yao na kuondoka jambo, lililozidi kumwongezea uchungu na kuonekana akizidi kulia mpaka alipokuja kutolewa eneo hilo na Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi wa chama hicho, Faustine Sungura.


Walimtoa eneo hilo na kumpeleka katika gari lake na kuondoka eneo hilo wakati huo ilikuwa saa 5:37 usiku.Wafuasi wa Kafulila washikwa huzuni


Hayo yakiendelea ndani nje kulikuwa na baadhi ya makada wa chama hicho waliokuwa kundi moja na Kafulila ambao walionekana kuwa na huzuni kubwa baada ya kupata habari hizo.


‘’Wamemfukuza..., wameshakiua chama ndio maana mimi nakuelezeni kila siku hiki sio chama, hakina demokrasia ya kweli, ni bora kwenda CCM tu kuliko hiki chama,’’ alisikika akisema mmoja wa makada hao.


Awali, wakati zikipigwa kura za kutokuwa na imani na Mbatia ulizuka mtafaruku baada ya wajumbe kushangazwa na kitendo cha kuwepo kwa wajumbe zaidi ya 60 wakati mkutano huo huwa na wajumbe wasiozidi 40.


Baadhi ya wajumbe waliibua hoja ya kutaka baadhi ya watu ambao hawafahamiki kujieleza na taratibu zitumike kuwatambua au kutowatambua.


Kutokana na hali hiyo kuibua mgogoro katika kikao hicho Rungwe pamoja na baadhi ya wajumbe walitoka nje ya mkutano huo, wakionyesha kutoridhishwa na maamuzi yaliyotolewa katika upigaji wa kura.


Habari hizo zilieleza kuwa Rungwe pia alijieleza sababu za yeye kuiandikia barua ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuiarifu kuwa kikao hicho hakikuwa halali


Awali, wakati mkutano ukiendelea habari za ndani kutoka katika mkutano huo zilieleza kuwa wakati ajenda mbalimbali zikijadiliwa Kafulila aliwasiliana na polisi na kuwaeleza kuwa katika mkutano huo kulikuwa na vurugu.


Mwananchi lilishuhudia polisi tisa wakiwa katika gari aina ya Landcruser wakifika katika Ukumbi huo saa 6:05 mchana na kuingia ndani ya ukumbi, ambao walielezwa hakukuwa na vurugu yoyote na wakatoka nje na kuondoka.


Ilipofika saa 6:45 polisi hao walirudi tena na kueleza kwamba, walipigiwa simu nyingine kwamba katika mkutano huo hali si shwari na safari hii walimhoji dereva wa Kafulila, Denis Kalikisha.


Wakati huo huo, chama hicho kimeomba kukutana na Rais Jakaya Kikwete kwa nia ya kutoa mawazo yake kuhusu mchakato wa kutungwa kwa Katibu Mpya ya Tanzania, kama ilivyoahidiwa kwa wananchi na mkuu huyo wa nchi.


Kafulila aliwahi kupinga kukutana na Rais Ikulu kwa madai suala zima la mchakato wa Katiba Mpya umekiukwa.


Lakini, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana ilisema Rais sasa amekubali ombi hilo la NCCR-Mageuzi.Mbali ya NCCR, Rais pia amekubali kukutana na Baraza la Taifa la Taasisi Zisizokuwa za Kiserikali (NGO’s), ambalo limeomba kukutana na kuzungumza nye.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment