Monday, December 19, 2011

Kafulila alivyosulubiwa NCCR- Mageuzi

DAVID Kafulila Mbunge kijana kutoka Jimbo la Kigoma Kusini juzi aliingia kwenye ukumbi wa mkutano akiwa na nguvu na matumaini ya kumsimamisha uongozi mwenyekiti wa chama chake cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, lakini mwisho, upepo ulivuma vibaya kuelekea upande wake na hatimaye akajikuta anasulubiwa na kisha kuvuliwa uanachama.


Kafulila ambaye alitokea Chadema na kujiunga NCCR- Mageuzi mwishoni mwa mwaka juzi na mwaka jana akafanikiwa kuingia bungeni baada ya kumwaga mgombea wa CCM, Kifu Gullamhussein , ni mwanasiasa kijana ambaye alianza kung’ara katika medani za siasa nchini kutokana na kusimamia hoja zenye maslahi ya umma kama Katiba Mpya, kupinga nyongeza ya posho za wabunge na kutaka wale ambao walisababisha hadi Dowans kupata tuzo ya zaidi ya Sh100 kuchukuliwa hatua.


Safari ya kumshughulikia Kafulila ilianzia Desemba 8 mwaka huu baada ya kuvuliwa wadhifa wa Katibu Mwenezi wa chama hicho na juzi, ilihitimishwa katika Ukumbi wa Proin ambako mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ulifanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi karibu saa tano usiku.


Gazeti hili liliwashuhudia wajumbe 64 wa mkutano huo wakifika katika ukumbi huo huku wakionekana kuwa na shauku ya kutaka kujua hatma ya chama hicho baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya Kafulila, Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia na Katibu wake Samwel Ruhuza.


Kafulila alifika katika ukumbi huo saa 2:00 asubuhi akiwa kwenye gari yake aina ya Toyota Altezza na moja kwa moja aliingia ndani baada ya mabaunsa zaidi ya 10 waliokuwa katika geti la kuingilia kumruhusu.


Mkutano huo ulianza rasmi mnamo saa 3:00 huku ukiongozwa na Dk Sengondo Mvungi, akisaidiwa na Ruhuza na Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Haji Ambari Khamis.


Katika mkutano huo, Mbatia alikuwa mmoja wa watuhumiwa ambao alipaswa kujibu tuhuma zake za kukifanya chama kama CCM B huku Kafulila akituhumiwa kuvujisha siri za chama nje ya utaratibu wa vikao. Moja ya tuhuma za Kafulila ni kueleza vyombo vya habari kwamba ameondolewa katika nafasi ya uenezi.


Lakini, hali ya mambo katika chumba cha mikutano ilianza kuvurugika ilipofika saa 8:00 mchana wakati wa kupigakura ya za kutokuwa na imani na Mbatia baadhi ya wajumbe walitoka nje ya ukumbi kwa maelezo kuwa baadhi ya wapiga kura hawakuwa wajumbe halali wa mkutano huo.


Habari hizo zilieleza kwamba, waliotoka nje walikuwa saba huku wakiongozwa na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Hashim Rungwe.


Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, baada ya hali kuwa shwari wajumbe hao walipokea na kujadili utetezi wa Mbatia. Tuhuma dhidi ya Mbatia zilitolewa na Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Mbwana Hassan pamoja na wengine 26 waliosaini hati ya kutokuwa na imani naye kwa madai kuwa ni CCM B.‘’Katika kupiga kura haki haikutendeka, wajumbe tulipiga kura kwa kunyoosha mikono na sio kura ya siri, pamoja na hayo Mbatia alionekana kuwa safi’’ alieleza mmoja wa wajumbe wa NEC wa chama hicho.


Hata hivyo, akizijibu shutuma hizo mbele ya waandishi wa habari jana, Ruhuza alisema kuwa mkutano huo ulitoa maazimio kwamba Mbatia yuko safi, hodari na shujaa wa chama.


‘’Wajumbe wote waliotoa malalamiko walijiondoa na Mbatia akawa safi hiyo ikiwa ni pamoja na hao waliokuwa wakimpinga awali,’’ alisema Ruhuza.


Baada ya kumalizika hoja ya Mbatia na kufanikiwa kuzima kile alichokuwa akikiita uasi dhidi yake, jioni ndipo ilipokuja hoja ya Kafulila.


Zamu hiyo ya Kafulila ilipokuja upepo ulionekana kubadlika ghafla ndipo alipopewa nafasi ya kujitetea kuhusu tuhuma zinazomkabili.


Habari hizo zilieleza kuwa Kafulila alipopewa nafasi ya kujieleza, alisema kama kweli kuna mvutano baina yake na Mbatia kinachotakiwa ni kukutana na kuzungumza chini ya usimamizi wa wazee wenye busara wa chama hicho.Habari hizo zilelieza zaidi kuwa Dk Mvungi wakati akitoa maelezo yake alisema kuwa wajumbe wanatakiwa kutumia busara katika uamuzi yao.


Hata hivyo, hali iliharibika zaidi kwani licha ya utetezi huo wa Kafulila, wanachama ndani ya ukumbi huo baada ya kuanza kupiga kura za kuwafuta uanachama makada wa chama hicho akiwemo Kafulila.


Habari zilieleza kuwa baada ya kuthibitisha upepo unavuma vibaya kwake na hakuna njia ya kutokea, Kafulila alikwenda kumwomba msamaha Mbatia huku akiwa amepiga magoti jambo ambalo liliwakera wajumbe ambao walimwita msaliti.


Lakini, wajumbe walipiga kelele, ‘’Anaigiza huyo muda wote alikuwa wapi?


Hata kujitetea kashindwa na amekuwa akijibu majibu ya mkato sasa ndio anakumbuka kuomba msahama, muongo huyo’’.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment