RAIS Jakaya Kikwete amekubali kukutana na kuzungumza na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu kutoka Dodoma jana jioni,ilieleza, kwamba
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea barua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kuomba viongozi wa chama hicho kukutana na Mheshimiwa Rais kuzungumzia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.
“Mheshimiwa Rais Kikwete amelipokea ombi hilo kwa furaha kwa sababu ni jambo jema.” Kutokana na kukubaliwa kwa ombi hilo, Ikulu ilieleza kwamba “Rais ameagiza mawasiliano yafanyike ili kupanga tarehe mwafaka ya kukutana na viongozi hao wa CHADEMA na kuzungumzia suala hilo.”
Majibu hayo ya Rais Kikwete yamekuja siku moja baada ya Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Taifa, Freeman Mbowe, kutangaza kuundwa kwa Kamati ndogo ya chama hicho kwenda kumuona Rais kumuelezea msimamo wao kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
Kamati hiyo ya watu saba na nafasi zao kwenye mabano, ni Freeman Mbowe (Mwenyekiti na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni), Said Arfi (Makamu Mwenyekiti Bara na Mbunge Mpanda Mjini), Said Issa Mohammed (Makamu Mwenyekiti Chadema Zanzibar) na Dk Willibrod Slaa (Katibu Mkuu).
Wengine ni Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari, wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho. Mbowe ndiye atakayeongoza kamati hiyo ndogo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu ya Chadema, Dar es Salaam, Mbowe alisema hatua hiyo inatokana na maazimio ya Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho ambayo imedai kuwa Serikali ya CCM haina dhamira ya kweli ya kuunda Katiba mpya.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema katika kikao hicho masuala mbalimbali yalizungumzwa, ikiwa ni pamoja na namna Muswada wa Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011 ulivyopitishwa na Bunge kuwa Sheria na kudai kwamba kitendo cha Chadema na wabunge wengine kususa mjadala, ni cha kishujaa kwa kuwa sheria hiyo haikufuata taratibu na kanuni za Bunge.
“Muswada uliopitishwa kuwa sheria na Bunge hauwatendei haki Watanzania, Kamati Kuu imejadili kwa kina na kuona kwamba ingawa Bunge limepitisha sheria, bado kuna fursa ya kitaifa kutokubaliana na hatua hiyo, ambayo haikuzingatia maoni ya wadau, tumeona CCM haina dhamira ya kuunda Katiba mpya,” alisema Mbowe.
Alidai kuwa CCM imekuwa ikipotosha hoja ya Chadema kuwa ingepewa ridhaa ingeanza mchakato wa kupata Katiba mpya ndani ya siku 100 na si kuunda Katiba ndani ya siku hizo, hivyo Kamati Kuu kuamua kuunda Kamati ndogo ya viongozi wa chama na baadhi ya wabunge kukutana na Rais Kikwete kwa nafasi yake ya urais na si uenyekiti wa CCM.
No comments:
Post a Comment