Wednesday, November 23, 2011

Ajali yaua mapadri 3 Ruvu

MAPADRI watatu wamekufa papo hapo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori eneo la Ruvu kwa Zoka, Bagamoyo mkoani Pwani.


Gari aina ya Toyota Land Cruiser namba T903ACQ mali ya Parokia ya Pugu, Dar es Salaam, lililokuwa likiendeshwa na Sylverio Ghell, mkazi wa Pugu, liligongana uso kwa uso na lori jana mchana.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, amesema, ajali hiyo ilitokea baada ya gari hilo lililokuwa likitoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kutaka kulipita lori mbele yake namba T181 BSQ na tela namba T286 ASY, na kugongana na lori namba T648 AET na tela namba T975 AYN.


Kamanda Mangu alitaja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Ghell, Corrab Trivelli, Lucino Baffivi na mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Andrew, wote raia wa Italia.


Mapadri hao ni wa Shirika la Wafrancisco Wakapuchini ambao baadhi yao hufanya kazi nchini.


Alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari la mapadri hao, likitaka kupita gari lingine.


Maiti wote wamehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi, Kibaha, Pwani.


Mkuu wa Shirika la Wafrancisco Wakapuchini, Padri Wolfan alisema mapadri waliokufa ni watatu waliokuwa wakitoka Kongwa, Dodoma kwenda Dar es Salaam.

2 comments:

  1. Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe, mbele yao nyuma yetu. wapumzike kwa amani. Amina

    ReplyDelete