Thursday, November 10, 2011

Tundu Lissu, Dk. Slaa walivyopandishwa kizimbani Arusha

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Wilbroad Slaa(kulia) na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wafuasi wao wakiwa mahakamani Novemba 8 mwaka huu.

Dk. Slaa ,Lissu na wafuasi wao kadhaa walipandishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa kutuhumiwa kufanya mkusanyiko wa watu kinyume na sheria.

Dk. Slaa pia anakabiliwa na shitaka lake peke yake la kudaiwa kutoa maneno ya uchochezi akiwa katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya NMC mjini Arusha.

Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Devotha Kamuzora,Mwendesha mashitaka wa Serikali Haruni Matagane aliiambia Mahakama hiyo kwamba kosa la kwanza na la pili linawakabili watuhumiwa wote 27 ambalo ni kufanya kusanyiko kinyume cha sheria na kutokutii amri ya Jeshi la Polisi.

Akisoma shitaka la pili, Haruna aliiambia mahakama hiyo kuwa, Dk. Slaa anadaiwa kutoa kauli zenye uchochezi akidai kuwa atahamasisha wafuasi wake waandamane hadi Magogoni Ikulu, Dar es Salaam kuhakikisha wanamg'oa madarakani Rais Jakaya Kikwete.

Kipengele kingine kilichotajwa na mwendesha mashitaka huyo ni Dk. Slaa kutangaza kwamba watakodisha ndege kwa ajili ya kumbeba Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Zuberi Mwobeji na kisha wampeleke Dar es Salaam kwa IGP ili kumuuliza kwa nini hadi sasa hajamhamisha kazi OCD huyo.

Katika kesi hiyo upande wa washitakiwa wote 27 unawakilishwa na mawakili wawili, Method Kimomogolo na Albert Msando.


Mawakili hao kwa pamoja waliiambia mahakama hiyo kuwa wateja wao walikuwa na watu wa kuwawekea dhamana kama mahakama hiyo itaona kuna umuhimu huo.

Hakimu Mkazi Devotha Kamuzura aliwaambiwa watuhumiwa kwamba dhamana yao ilikuwa wazi lakini kwa masharti ya kila mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili na ahadi ya dhamana ya shilingi milioni tano.

Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 22, mwaka huu mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment