Thursday, November 10, 2011

Sauda Mwilima avishwa pete ya uchumba

Sauda Mwilima na Kauli Juma siku walipovishana pete ya uchumba jijini Dar es Salaam.

PENZI la siri kati ya mtangazaji runinga ya Star TV, Sauda Mwilima na mpenzi wake wa siku nyingi aitwaye Kauli Juma lipo hadharani baada ya jamaa huyo kuamua kutangaza nia na kumvalisha pete ya uchumba.

Awali, waalikwa wa shughuli hiyo walitaarifiwa kwamba sherehe ilikuwa ni ‘birthday’ ya mtangazaji huyo, hivyo wahudhuriaji hawakujua kabisa kuwa kuna tukio kubwa na muhimu kwa Sauda.

Tukio la Sauda kuvalishwa pete lilifanyika majira ya saa 6 na dakika zake za usiku, baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi wa shampeni iliyokuwa imeandaliwa kama changa la macho kwa wageni ambao walijua ni kwa ajili ya sherehe ya kuzaliwa.


Watu wakionekana kuchoka, wakati wakipata shampeni, mshereheshaji wa shughuli hiyo, Christina Manongi a.k.a Sintah alisimama na kuwaomba radhi wageni kwa kuwa kulikuwa na zaidi ya sherehe ya kuzaliwa.


“Mabibi na mabwana, tunawashukuru sana kwa uvumilivu wenu, lakini lazima tuombe radhi, hii si birthday pekee isipokuwa leo ni siku muhimu zaidi kwa Sauda ambaye atavalishwa pete ya uchumba na Kauli.


“Kwa nafasi hii, naomba kuwakaribisha wasogee hapa ili kila mmoja ashuhudie tukio hili muhimu,” alisema Sintah na ukumbi mzima kulipuka kwa vigelele na shangwe.

Watu hawakuamini walichosikia, waliendelea kushangilia wakati Sauda na Kauli wakisogea mbele kwa ajili ya kukamilisha tendo hilo muhimu kabla ya ndoa.


Kauli akiwa katika harakati za kunyanyua mkono wa Sauda tayari kwa kumvalisha pete, ghafla alitokea babu yake Sauda, aliyetambulishwa baadaye kwa jina la mzee Zahoro Selema na kupinga tendo hilo.


“Haiwezekani ninyang’anywe mke kirahisi namna hii? Huyu bwana kama anataka nimwachie huyu mwanamke lazima anipe kitu kidogo...anipooze kwanza,” alisema mzee Selema na watu wakaangua vicheko.


Ili kumaliza utata huo ambao ulikuwa na msingi wa utani, Kauli alizama mfukoni, alipoibuka alikuwa na shilingi 15,000 akamkabidhi mzee huyo na ratiba ikaendelea kama ilivyopangwa.

Katika hafla hiyo, mastaa kedekede walitia timu, baadhi yao ni Jacqueline Wolper, Wema Sepetu, Maimartha Jesse, Milard Ayo, Janeth Mwenda (aliyekuwa mtangazaji wa Radio One), Steve Nyerere, Juma Chikoka, Husna Mauld ‘Sajenti’, Taji Liundi na wafanyakazi kadhaa wa Star TV.


Mastaa wengine ni Linex, Shaban Katwila ‘Q Chilla’ Mrisho Mpoto ‘Mjomba’ na Naseeb Abdul ‘Diamond’ ambao walipiga shoo safi iliyosindikiza hafla hiyo iliyofana.


Picha, Habari kwa hisani ya blog ya freebongo

No comments:

Post a Comment