Thursday, November 3, 2011

Shule yatumia mitaala ya Kikongo Dar, wanafunzi hawajui kusoma, kuandika Kiswahili

KWA miaka 12 sasa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Bande Ndagundi, amekuwa akiendesha shule nchini kwa mtaala wa Kikongo tena bila usajili.


Kutokana na hali hiyo, ambayo ni dhahiri ilinyamaziwa kwa miaka yote hiyo, hatimaye jana, Serikali imeifunga rasmi shule hiyo ambayo inajumuisha madarasa ya awali, msingi na sekondari kwa jina la Ecole Francophone Ces Grands Lacs (Shule ya Kifaransa) Sinza.


Shule hiyo iliyoko Sinza, Kinondoni, Dar es Salaam, imekuwa ikiendesha masomo yake kwa Kifaransa, huku mitihani yake kuanzia chekechea hadi kidato cha sita ikitungwa DRC.


Kwa mujibu wa habari zilizopo, shule hiyo ilikuwa ikiendesha shughuli zake katika eneo lisiloruhusiwa kisheria, nyuma ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God, la Askofu Zakari Kakobe, maeneo ya Mwenge.


Akiifunga rasmi shule hiyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kugundua kwamba inaendesha masomo yake kinyume na taratibu za serikali ya Tanzania.


“Kwa kweli tulitakiwa kumshitaki na kumfunga mmiliki wa shule hii, na sasa tunaifunga shule hii rasmi,” alisema Naibu Waziri mbele ya wanafunzi na walimu.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, shule hiyo ilikuwa ikifuata taratibu na mfumo wote kutoka Congo bila kusajiliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini.


“Tunajua, kwamba wanafunzi mmeshalipa ada zenu, mnachotakiwa kufanya sasa ni kumshitaki mmiliki na kudai fedha zenu.


“Na pia natoa mwito kwa wananchi wote nchini, kuwa makini na shule za aina hii, kwa sababu zinaweza kuwaibia fedha zenu bure na mkaishia hewani,” alisema.


Shule hiyo hadi inafungwa, ilikuwa na wanafunzi 200 kuanzia ya awali hadi kidato cha sita, na wengi wao hawajui kuongea wala kuandika Kiswahili.


Hata hivyo, Naibu Waziri alimtaka mmiliki wa shule hiyo kuhakikisha watoto wote wanaendelea na elimu na awatafutie shule nyingine.


Mulugo alisema kuna shule kama hiyo inayoendesha masomo yake yote kwa Kifaransa mkoani Kigoma, ambayo inatambulika na Serikali ya Tanzania.


“Hakikisheni wanafunzi hawa wanaendelea na shule, fanyeni utaratibu wa kuwapeleka Kigoma, ambako kuna shule kama hii inayotambuliwa na Serikali,” alisema.


Mkaguzi Mkuu wa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Catherine Baiynt, alisema waliigundua shule hiyo baada ya kuifuatilia kwa muda mrefu.


“Kwa sasa tuna utaratibu wa ukaguzi wa shule zote zilizosajiliwa na zisizosajiliwa, hivyo sisi kwa upande wetu wa Dar es Salaam, tumeigundua shule hii,” alisema.


Kwa mujibu wa Catherine, shule hiyo ilianza mwaka 1999 ikijulikana kama Elite kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa Ecole Trancphone.


Naye Ndagundi alisema waliianzisha kwa malengo ya kusaidia watoto wa wakimbizi wa Burundi, Rwanda na DRC.


“Kwa kweli tulianzisha shule hii kwa malengo ya kuwasaidia watoto wa wakimbizi, lakini wazazi wengi (wasio wakimbizi) wakaipenda na tukaanza kuwasajili,” alisema.


Aliongeza, kwamba kwa sasa watafuata taratibu zote za Serikali ili kuisajili iendelee na shughuli zake na kutoa huduma ya elimu.


Hata hivyo, alipoulizwa na Waziri kuhusu hatima ya wahitimu wa shule hiyo baada ya kidato cha sita mmiliki wa shule hiyo, alikosa majibu.


Kwa hali ilivyokuwa, wanafunzi wote waliokuwa wakimaliza shule ya awali, hawakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kuendelea na sekondari katika shule hiyo mpaka kidato cha sita.


Chanzo: Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment