Friday, November 4, 2011

Shein- Mimi si Waziri, sijaudhalilisha urais Zanzibar

RAIS wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein amesema alikula kiapo kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano ili kutekeleza matakwa ya Katiba, mazingira ambayo yatasaidia kuimarisha zaidi muungano.

Alisema hayo jana alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari wa Tanzania Ikulu, mjini Zanziba akitimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani Novemba 3 mwaka jana.

Alisema matakwa ya Katiba yanatamka wazi kwamba Rais wa Zanzibar
atakula kiapo kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Muungano.

“Mimi si wa kwanza kula kiapo kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri…wala hadhi ya urais wa Zanzibar haijashuka … Rais Karume (Amani Abeid) alifanya hivyo mara mbili na nilimshuhudia nikiwa Makamu wa Rais pale Ikulu Dar es Salaam … ndiyo matakwa ya Katiba yanavyosema si utashi wangu,” alisema.

Alisema kiapo chake ni kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri Muungano wa Tanzania na si waziri asiye na wizara maalumu kama inavyodhaniwa na kwamba hadhi yake ya Rais wa Zanzibar iko pale pale.

Dk. Shein alisema hayo ni matokeo ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 yaliyotokana na mfumo wa vyama vingi vya siasa, ambayo yaliondoa nafasi ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Alisema utaratibu huo upo tangu zamani na wala yeye hakula kiapo ili kuvunja Muungano au kudhalilisha nafasi ya urais wa Zanzibar.

“Wapo watu wanasema mimi nimeidhalilisha nafasi ya urais wa Zanzibar kwa kula kiapo kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania … si kweli hata kidogo nadhani watu wanatakiwa kufahamishwa na kuifahamu Katiba,” alisema Dk. Shein.

“Kule kuna mambo yanayohusu Zanzibar na yanatakiwa ufafanuzi au uamuzi sasa kama wewe haupo, watu wanapitisha tu … lakini kama upo kwanza unaulizwa na kutakiwa ushauri wako,” alisema.

Mapema Dk. Shein alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaendelea vizuri na kupata mafanikio makubwa licha ya changamoto.

Kuhusu mgawo wa misaada alisema misaada inayotolewa na mashirika ya kimataifa ya asilimia 4.5 katika Jamhuri ya Muungano, Zanzibar inafaidika moja kwa moja.

“Tunafaidika na fedha za misaada zinazotolewa na mashirika ya kimataifa ikiwamo gawio la asilimia 4.5… hata gawio letu katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tunalipata kwa mujibu wa makubaliano ya mgawanyo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), “ alisema.

Aidha, alisema kero za Muungano zinaendelea kupatiwa ufumbuzi wake chini ya Kamati inayoongozwa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, ambapo matarajio mazuri ni makubwa.


Chanzo: Gazeti la HabariLEO

No comments:

Post a Comment