Monday, November 7, 2011

Prince Charles, Camilla wapo Dar es Salaam

Picha ya maktaba

MTOTO wa Malkia wa Uingereza, Elizabeth II, Prince Charles amewasili nchini kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Jakaya Kikwete.


Prince Charles aliyefuatana na mkewe Camilla, waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana jioni, kwa ndege ya Uingereza, CS-TFY, wakitoka Afrika Kusini na kulakiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.


Baada ya mapokezi hayo, walitumbuizwa na ngoma za asili ya nchini pamoja na muziki wa matarumbeta kutoka kwa vikundi vilivyoandaliwa maalumu kwa ajili yao.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Ubalozi wa Uingereza nchini, Mark Polatajko, ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.


Awali, Polatajko alisema kuwa Prince Charles, pamoja na kutembelea miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Shirika la Misaada ya Uingereza (DFID), pia atazungumzia kazi za Mfuko wa Hifadhi ya Asili Duniani (WWF) katika kulinda jamii ya wanyamapori iliyo hatarini kutoweka, pamoja na masuala ya uhifadhi.


Ratiba iliyotolewa jana ilionesha kuwa Mwana huyo wa Mfalme atakuwa na mazungumzo na Rais Kikwete Ikulu ya Dar es Salaam leo asubuhi, kabla ya kwenda Karimjee kupokea taarifa ya mafanikio ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, inayoanza kuadhimisha wiki yake ya miaka 50 ya Uhuru.


Akiwa Karimjee, Prince Charles ataelezwa historia ya jengo hilo na kuzindua stempu zenye kuashiria maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru na kisha kutembelea Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Ngome ambapo atakagua gwaride.

Baada ya shughuli hiyo, Prince Charles aliyepo nchini kwa mara ya pili, atahudhuria semina ya uvuvi endelevu na baadaye kutembelea makao makuu ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama).


Baada ya shughuli za Wama atakwenda Kigamboni, nje kidogo ya Dar es Salaam kukagua mradi wa maji unaofadhiliwa na nchi yake, kabla ya kuelekea Zanzibar kesho.


“Ziara yake itahusisha mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na kumalizika Novemba 9, mwaka huu,” ilieleza sehemu ya ratiba hiyo.

Chanzo:Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment