Wednesday, November 30, 2011

Mukama- CCM haikukurupuka

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama amesema uamuzi wa chama hicho kuwawajibisha watuhumiwa wa ufisadi haukufanywa kwa kukurupuka, bali ni wa makini uliowekwa katika mpango wa utekelezaji.


Katika mpango huo, Mukama aliyekuwa akirejea hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ya kujivua gamba na kuoanisha na mkakati wa utekelezaji, alisema walikubaliana iundwe Tume ya Udhibiti na Nidhamu ambayo itapewa mamlaka ya kumwajibisha mwanachama mwenye kosa bila kusubiri vikao vya chama.


Akizungumza jana katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba Dar es Salaam, Mukama alisema uamuzi wa Tume hiyoyenye watu wachache, utasaidia kuondoa uwezekano wa kufanya uamuzi wake kuwa wa kisiasa zaidi na kusababisha mwenye kosa kupita bila kuadhibiwa.


“Tume ina mamlaka makubwa, inamaliza kila kitu hapo hapo, itaamua na kutoa adhabu… itapunguza kufanyia siasa kosa na mtuhumiwa kupita bila kuadhibiwa na asiye na kosa akaadhibiwa,” alisema Mukama.


Alifafanua kuwa kosa hilo, linaweza kufanywa katika vikao vyenye watu wengi na ndiyo maana Kamati Kuu iliomba kukasimiwa madaraka ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, lakini pia itasaidia kumfanya aliyeadhibiwa kuwa na nafasi ya kukata rufaa.


Alitoa mfano wa Mahakama ya Rufaa inapomhukumu mtuhumiwa kuwa inaanza na jopo la majaji watatu, watu wachache kwanza na mtuhumiwa asiporidhika, anakata rufaa kuomba kikao cha majaji wanane.


Alisema Tume hiyo inachukua nafasi za Kamati za Usalama na Maadili ambazo alisema hazina uwezo wa kuamua na badala yake zinapeleka taarifa ngazi za juu.


Mukama alisema, kikao cha Nec ya CCM kilichomalizika Dodoma wiki iliyopita, hakikumtuhumu wala kumsafisha mtu na anashangaa kusikia waandishi wa habari wakisema kuna mtu kashinda.


Badala yake Mukama alisema Kamati Kuu ya CCM katika kikao hicho, iliomba kukasimiwa madaraka ya Nec ya kuwaadhibu viongozi wake, ambao ni watuhumiwa wa ufisadi waliokataa kuchukua uamuzi wenyewe. Alipotakiwa awataje watuhumiwa wa ufisadi alikataa kutaja majina na badala yake akasema: “Hizi ni zama za siasa safi.


“Katika siasa kuna kitu kinaitwa mtazamo wa kijamii na kipimo kimoja kinachotumika ni je, wenzako wanakuonaje? Kama katika watu 10, saba wanasema hufai kuwa kiongozi unaitwa aliyekataliwa. “Yupo ambaye hatajwi kwa chochote, si kwa mabaya au mazuri hiyo inaitwa kutengwa kijamii, huyo pia hafai kuwa kiongozi,” alisema Mukama.


Akifafanua hoja hiyo bila kutaja majina, Mukama alisema kila sehemu CCM inaonekana imehama kutoka kwa wanachama na kuwa ya matajiri.


Hata hivyo katika Mkutano wa NEC, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa alikaririwa akilalamika kuwa amekuwa akiitwa fisadi na wanachama wenzake ambao wanatumia fedha za chama kumtukana.


“Sasa unataka tusubiri mpaka uone viongozi wote ni matajiri ndipo ujue chama kimetekwa na matajiri?” Alihoji Mukama.


Mukama alisema ushahidi walionao ni wa kura za maoni za ndani ya CCM zilizofanyika katika uchaguzi mkuu uliopita, ambapo alisema ziliwafumbua macho.


Alitoa mfano wa uchaguzi wa kata za Kirumba, Kitangiri na Nyamanoro jijini Mwanza, ambazo washindi wa pili wa kura za maoni za CCM, walihamia Chadema na kushinda.


“Tumejiuliza kwa nini namba moja wetu waangushwe na namba mbili, hizi ni namba moja kweli?” Alihoji.


Alitoa mfano mwingine wa Dar es Salaam katika majimbo ya Ubungo na Kawe, akifafanua kuwa wagombea wa CCM walioshindwa katika majimbo hayo, walikataliwa na wanachama katika kura hizo.


Alisema mgombea wa CCM Ubungo alipata asilimia 34 ya kura za wanachama, maana yake alikataliwa na asilimia 66 ya wanachama na walipokwenda katika uchaguzi wakashindwa.


Kawe kwa mujibu wa Mukama, mgombea wa CCM alipata asilimia 22 ya kura za maoni na maana yake alikataliwa na wanachama kwa asilimia 78 na katika uchaguzi mkuu alishindwa.


Kigamboni ambako alisema walifanyakazi kubwa mpaka mgombea wa CCM akashinda katika uchaguzi mkuu, walipata shida kwa kuwa mgombea huyo katika kura za maoni, alipata chini ya asilimia 20, maana yake zaidi ya asilimia 80 ya wanachama walimkataa.


Katika Jimbo la Ilala kwa mujibu wa Mukama, mgombea wa jimbo hilo akamtaja jina la Zungu (Musa Azzan), alipata asilimia 84 ya kura za maoni na akashinda kwa asilimia 70.


Kutokana na hilo Mukama alisema kwa sasa wanafikiria mshindi wa kura za maoni awe amepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote.


Chanzo: Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment