MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa, imemhukumu Ernest Fredrick (38), mkazi wa Nsemulwa Migazini mjini humo, kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kujaribu kumbaka mama yake mzazi.
Mwendesha Mashitaka, Inspekta Timothy Nyika, alidai mahakamani hapo, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 29, mwaka jana nyumbani kwa mama yake huyo.
Ilidaiwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Richard Kasele, kuwa siku ya tukio, mshitakiwa aliingia ndani ya nyumba ya mama yake na kumshika kwa nguvu akilenga kufanya naye mapenzi.
Katika kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi mjini humo, ilidaiwa pia kuwa pamoja na mama kukataa, mwanawe huyo aliendelea kumshika kwa nguvu na hatimaye kumvua nguo.
Mwendesha Mashitaka alidai kuwa baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, mama alipiga mayowe akiomba msaada na majirani walifika na kumkuta mtoto akiwa amemlalia mama yake huku mama akiendelea kupiga kelele.
Aliendelea kuiambia Mahakama hiyo, kwamba majirani walimwokoa mama ambaye alijieleza alichotaka kufanyiwa na mwanawe huyo ndipo majirani haop wakamkamata mtuhumiwa na kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi cha Mpanda.
Hakimu Kasele alisema aliridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka pasipo shaka yoyote na kudhihirisha kuwa mshitakiwa alitenda unyama huo.
Mshitakiwa alipotakiwa na Mahakama ajitetee, aliomba apunguziwe adhabu kwa maelezo kwamba bado ni kijana.
Ombi ambalo lilipingwa na Mwendesha Mashitaka kwa maelezo kuwa kama aliweza kumfanyia unyama huo kwa mama yake mzazi kwa watu wengine itajkuwaje.
Hakimu Kasele alimhukumu kifungo cha miaka 20 jela.
Chanzo: Gazeti la HABARILEO
No comments:
Post a Comment