Monday, November 14, 2011

Lema kuitikisa Arusha leo

JIJI la Arusha na viunga vyake leo linatarajiwa kujaa shamrashamra za kumpokea Mbunge wake, Godbless Lema anayetarajiwa kurejea uraiani kutoka mahabusu Gereza Kuu la Kisongo alikokwenda kwa hiari yake kupinga kile alichokiita manyanyaso ya jeshi la polisi dhidi yake na kuonyesha ujasiri wa kutoogopa jela.


Oktoba 31, mwaka huu, Lema na wenzake 18 walifikishwa mahakamani wakidaiwa kufanya kusanyiko lisilo halali na kukaidi amri ya polisi iliyowataka watawanyike yeye na wenzake.


Walikamatwa na kufikishwa mahakamani na kudhaminiwa lakini Lema akikataa dhamana akisema ameamua kutangulia gerezani kudhihirisha kwamba haogopi gereza.


Jana, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Mkoa wa Arusha Ephatah Nanyaro alisema Lema atapokewa na wafuasi wake kuanzia eneo la mahakama na watatembea kwa miguu hadi sehemu maalumu aliyopangiwa kwa ajili ya kuzungumza na wananchi na wapiga kura wake.


“Tunaliomba jeshi la polisi lisitafsiri mapokezi haya kama maandamano. Hatukusudii kuandamana. Tutakachofanya ni kumpokea mbunge na shujaa wetu na tutadhibiti ulinzi na usalama wetu wenyewe ingawa pia hatutakaa ulinzi wa polisi ambayo ni haki yetu kikatiba kama raia wema na walipa kodi wa nchi hii,” alisema Nanyaro.


Alipoamua kwenda gerezani Lema alisema: “Leo nimeamua kwa hiari yangu kutangulia magereza. Watakaotubeza tuwasamehe kwa sababu wanahitaji ukombozi wa kifikra. Watakaotuunga mkono na kutuhurumia tuwafundishe ujasiri wa kutoogopa jela wala magereza katika mapambano ya kutafuta haki, uhuru na utu wa mwanadamu,” alikaririwa Lema katika waraka alioutoa kwa wafuasi wakesiku alipokwenda mahabusu.


Uamuzi huo wa Lema ulifuatiwa na mtiririko wa matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani katika jiji hilo muhimu kwa shughuli za utalii, ikiwamo mgomo wa daladala na pikipiki.


Waraka wa kuhamasisha mgomo huo ulioandaliwa na kusambazwa na watu wasiojulikana ulidai kuwa pia ulikusudiwa kumpinga Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Zuberi Mwombeji anayedaiwa kukejeli baadhi ya watu.


Hata hivyo, mgomo huo ulioanza saa 2:00 asubuhi na kudumu kwa saa tatu, ulidhibitiwa na polisi huku watu zaidi ya 30 wakitiwa mbaroni, kati yao 25 walifikishwa mahakamani.


Baada ya tukio hilo, hamaki kubwa ilitokea Oktoba 7, mwaka huu baada ya mahakama kugoma kutoa hati ya kumtoa Lema gerezani ili kukamilisha masharti ya dhamana iliyotolewa na Hakimu Judith Kamara, kitendo kilichosababisha kukamatwa kwa viongozi wa kitaifa wa Chadema akiwamo Katibu Mkuu, Dk Willibroad Slaa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe baada ya Jeshi la Polisi kufanya operesheni ya kushtukiza kuwatawanya pamoja na wafuasi wao waliokuwa wamepiga kambi kwenye Uwanja wa NMC Unga Limited.


Hivi sasa Mbowe, Dk Slaa na watu wengine 26 wanakabiliwa na kesi mahakamani kuhusiana na mkesha huo na kufanya idadi ya kesi zilizofunguliwa dhidi ya viongozi na wanachama wa Chadema tangu kuanza kwa mgogoro wa Arusha mapema mwaka huu, kufikia Sita.


Tamko la Polisi Jeshi la polisi mkoani Arusha, jana lilitoa tamko kuhusiana na mbunge huyo kufikishwa mahakamani na kupewa dhamana kuwa halitarajii kuwapo kwa vurugu.Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alisema wanatarajia kuwa leo baada ya Lema kupewa dhamana hakutakuwa na jambo ambalo si la kawaida na ataondoka mahakamani bila matatizo.


Alipotakiwa kuelezea kama watawatawanya wafuasi wa Chadema endapo wataamua kumsindikiza kwa miguu mbunge huyo kama ilivyotangazwa alisema hawezi kuzungumzia hatua zitakazochukuliwa kabla ya kosa kutendeka.


“Ngoja tuone kesho (leo) hali itakuwaje, siwezi kusema leo kama tutawatawanya au la. Ila sisi tunaamini mbunge akipewa dhamana ataondoka mahakamani kama kawaida ya watuhumiwa wengine bila vurugu,” alisema Mpwapwa.


Hata hivyo, ilielezwa kuwa polisi na baadhi ya viongozi wa Chadema walifanya mazungumzo ili kuhakikisha Jiji la Arusha linakuwa shwari mara baada ya Lema kupata dhamana leo.


Kamanda Mpwapwa alisema jeshi hilo halina nia ya kukabiliana au kujenga uhasama na wafuasia wa chama chochote cha siasa kikiwemo Chadema pale wanapofanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, lakini alionya kuwa hawatasita kudhibiti uvunjifu wowote wa amani na utulivu unaofanywa na mtu, kundi au chama chochote cha siasa.


Jiji la Arusha limekuwa likigubikwa na vurugu za kisiasa mara kwa mara tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambao pamoja na mambo mengine, uliacha majeraha yanayotokana na matokeo ya uchaguzi wa umeya ambayo Chadema kimekuwa kikiyapinga.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment