Thursday, October 27, 2011

Waliokufa ajali ya basi kuzikwa kaburi moja

WATU 12 walioteketea kwa moto katika ajali ya basi la Deluxe Coach iliyotokea Misugusugu mkoani Pwani juzi alasiri, watazikwa leo kwenye kaburi moja katika eneo la Air Msae mjini Kibaha.


Eneo hilo ndipo walipozikwa watu waliopata ajali ya basi la Air Msae lililokuwa likitokea Arusha kuja Dar es Salaam miaka ya 1990.


Uamuzi huo umefikiwa jana katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani, iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mwantumu Mahiza kutokana na miili hiyo kuharibika kabisa na kushindwa kutambulika.


Akizungumzia mazishi hayo jana, Mahiza alisema kabla ya maziko, miili ya watu hao itachukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo vya vinasaba (DNA) ili vifanikishe utambuzi wao.


Taarifa kutoka Hosptali Teule ya Tumbi, zilieleza kuwa hata wananchi waliokwenda kujaribu kutambua ndugu zao, walishindwa kufanya hivyo kutokana na kuharibika kwa miili hiyo ambayo baadhi imekuwa majivu.


Mahiza aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kufanikisha kuwatambua ndugu zao, kwa kupeleka vitu kama nguo ambazo ndugu zao walizitumia siku chache kabla ya ajali hiyo.


"Tunaomba wananchi walioondokewa na ndugu zao katika ajali hii watoe ushirikino kwa kuleta vitu kama soksi, shati, khanga au viatu alivyokuwa anatumia ndugu yao hivi karibuni ambavyo havijafuliwa ili visaidie kutambuliwa baada ya kupimwa kwa njia ya vinasaba,” alisema Mahiza.


Ofisa Habari wa Hosptali Teule ya Tumbi, Rose Mtei alisema, majeruhi waliofikishwa katika hospitali hiyo ni 36, 35 waliruhusiwa na mmoja aliyelazwa anaendelea vizuri.


“Kutokana na ajali hiyo ndugu wamefika kujaribu kutambua miili hiyo lakini haikuwezekana kutokana na kuharibika vibaya na wengi wamekuwa majivu, kwa sasa tunasubiri tamko la uongozi wa Mkoa ili kujua mazishi yatakuwa wapi,” alisema Mtei kabla ya tamko la Mahiza.


Kati ya miili hiyo 12, ni miili mitano tu ambayo inaonekana kama miili ya watu lakini haitambuliki ya nani na miili mingine imekuwa majivu kabisa.


Kwa mujibu wa shuhuda wa ajali hiyo, Anna Amani, basi hilo baada ya kupinduka lililipuka, watu waliokuwa ndani walishindwa kutoka, uokoaji ukawa mgumu na hivyo ni abiria wachache tu waliweza kujiokoa.

Alisema basi hilo lililala kiubavu huku likiwaka moto, baadhi ya abiria walitoka kupitia madirishani, wengine wakishindwa kufanya hivyo na kukutwa na mauti.


Chanzo: HABARILEO

No comments:

Post a Comment