Thursday, October 27, 2011

Wafanyakazi TICS waendelea na mgomo

MGOMO wa wafanyakazi wa Kampuni ya TICS katika Bandari ya Dar es Salaam, jana uliingia yake siku pili baada ya uongozi wa kampuni hiyo kushindwa kutatua madai yao.


Kama ilivyokuwa juzi, wafanyakazi hao jana walikwenda kazini, lakini hawakufanya kazi.Walikuwa wakiingia ndani na kutoka nje kwa jazba, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa getini ili kuzuia waandishi wasiingie.


Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na gazeti hili nje ya ofisi hizo, walisema wameazimia kugoma hadi madai yao yatakapotekelezwa.


"Tumeamua kugoma hadi kieleweke, tunamtaka Waziri wa Uchukuzi aje asikilize madai yetu," alisema mmoja wa wafanyakazi hao na kutaja baadhi ya madai hayo kuwa ni ubaguzi katika upatikanaji wa maslahi mbalimbali.


Alan Ally alisema mgomo huo unatokana na kutotekelezwa kwa matakwa ya mkataba wa kazi unaoitaka kampuni hiyo kuwapa hisa watumishi baada ya kufanya kazi kwa miaka kumi.


“Mkataba tuliochukuwa hapa ni kuwa baada ya miaka 10 tunapaswa kupewa hisa na mshahara unaongezeka, sasa miaka kumi imeisha na jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho tulipowafuata wahusika walisema hisa zipo lakini zinauzwa na kututaka kila mtu atoe million 16,”alisema.


Mgomo huo umesababisha shughuli za Kitengo cha Kupakua na Kupakia Makontena katika Bandari ya Dar es Salaam, kusimama, huku madereva wa magari waliokuwa wamefika kuchukua mizigo yao bandarini wakilalamika kuathiriwa na mgomo huo.


Wafanyakazi hao walisema wanafanyakazi kubwa ikilinganishwa na mshahara wa Sh500, 000 kwa mwezi kwa mfanyakazi wa kima cha chini wakati mzungu wa kima cha chini analipwa Dola 30,000 kwa mwezi.


Kama ilivyokuwa juzi, hakuna kiongozi yeyote wa TICS aliyepatikana jana kuzungumzia suala hilo na jitihada za gazeti hili kumpata msemaji wake Benjamin Thomson hazikuzaa matunda baada ya yeye kutosema chochote.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment