Thursday, October 20, 2011

Lowassa ajibu mapigo

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema, amechoka kukashifiwa na kuanzia sasa hatakubali kuchafuliwa.


Amesema, mtu yeyote au chombo chochote cha habari na atakayefanya hivyo, ajiandae kukabiliana na mkono wa sheria.


Lowassa alitoa onyo hilo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake katika Kijiji cha Ngarash Wilaya ya Monduli, Arusha.


“Imetosha. Sasa nimeamua kukabiliana na yeyote atakayenichafulia jina na kunizulia mambo ya uongo. Nitatumia vyombo vya sheria na tayari nimewaelekeza mawakili wangu kufanya hivyo,” alisema,


“Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu sasa, nimeamua kuanza kuchukua hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria ambazo naamini zitatoa majibu sahihi dhidi ya wale wote walio nyuma ya ajenda hizi chafu kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawia ndani ya chama changu na kwa jamii nzima ya Watanzania ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya kizushi na wakati mwingine ya hatari dhidi yangu,” alisema.


Alisema tayari amepanga kuanza kuwasiliana na kuwasilisha malalamiko yake kwa mamlaka husika zinazosimamia mienendo ya kimaadili na weledi wa kitaaluma wa vyombo vya habari kama vile Msajili wa Magazeti na Baraza la Habari Tanzania (MCT).


“Kama hiyo haitoshi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu nimeshaanza kufikiria na kujipanga kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa habari na wahariri ambao kwa makusudi wameamua kutumia vibaya uhuru wa habari ambao serikali imeutoa. Naamini sote tunakubaliana kuwa uhuru usio na nidhamu ni fujo.


Katika mkutano huo, Lowassa alikanusha madai kuwa hivi sasa yeye na baadhi ya wanaCCM, wanakusanya taarifa na vielelezo vya mabaya ya Rais Kikwete ili kuyawasilisha kwenye vikao vya chama.


Alisema katika mkakati huo, mahasimu hao wamekuwa wakivitumia baadhi ya vyombo vya habari na kufikia hatua ya kudai kuwa ameanza kuandaa orodha ya kile anachokiita madhambi ya Rais Kikwete ambayo wanadai kuwa amepanga kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.


Alisisitiza kuwa ni jambo lisiloingia akilini kumhusisha yeye na kile kinachoitwa mkakati wa kumhujumu Rais Kikwete au CCM ambacho alisema ni Mbunge anayetokana na chama hicho na kiongozi wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.


“Kuhusu hili, napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiita mabaya au madhambi ya Rais, sina na wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete,” alisema na kuongeza:


“Siyo kweli. Nampenda, namwamini na kumheshimu Kikwete ambaye urafiki wetu haukuanzia barabarani kama baadhi wanavyodhani. Kwanza sijui mabaya ya mheshimiwa Rais. Najua mazuri yake mengi lakini siyo mabaya, hivyo sina nia ya kuyatafuta. Siwezi kumhujumu Rais wala chama changu. Naamini hata mheshimiwa Kikwete pia hawezi kuamini uongo huo.”


Alisema awali, alikuwa akiyapuuza madai mengi yanayoelekezwa kwake lakini amelazimika kuvunja ukimya kwani uongo ukizungumzwa mara nyingi bila maelezo sahihi kutolewa, unaweza kugeuka kuwa ukweli na watu wakauamini.


Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment