Wednesday, September 14, 2011

Waokolewa wakiwa kwenye friji, mzoefu akutwa anakula biskuti

Mmoja wa waokoaji waliokuwa wa kwanza kufika eneo ilipozama meli ya MV Spice Islanders, katika Bahari ya Hindi visiwani Zanzibar Septemba 10 mwaka huu, Makame Mkadara maarufu kwa jina la Kilo, amesema, baada ya kufika eneo la tukio walishuhudia matukio ambayo hawakuyatarajia.

Mkazi huyo wa Nungwi ilipozama meli hiyo amesema, “Katika boti niliyokuwa nimepanda sisi ndiyo tuliokuwa wa kwanza kufika mahali meli ilipozamia kwani tulifika saa 1.05 asubuhi ukiwa ni muda mfupi baada ya helkopta ya waokoaji kuwasili hapo.


“Tulipofika tu, jambo la kwanza tuliwazungukia abiria wote mahali walipokuwa wamejikusanya katika maeneo tofauti tofauti na kuwapa moyo kwamba tumeshafika kwa ajili ya kuwaokoa.


“Tukawa tunawaambia wasiwe na wasiwasi, waokoaji na meli zinakuja kwa kasi kwa hiyo wasiwe na hofu.


“Pamoja na kauli za matumaini tulizokuwa tukiwapa, kila tuliyekuwa tukimuona kwamba amezidiwa, tulikuwa tukimuokoa.

‘Kwa mfano mtu wa kwanza kumuokoa alikuwa ni binti mmoja wa kama miaka 13 hadi 14 hivi ambaye tulimuokoa saa 1.08 hivi.


“Baada ya kumuokoa binti huyo ambaye alikuwa ameshikilia gunia lililokuwa limejaa kandambili, akatuambia kifua kinamuuma sana na tumbo limejaa kwa sababu alikuwa amekunywa maji mengi.

“Mbele yetu tuliona friji moja, tukaamua kulifuata,tulipolikaribia, tukakuta likiwa limefunguliwa mlango, ndani tukawakuta watu wawili, mmoja alikuwa mzee wa makamo na kijana mdogo wa kama miaka 12 hivi, wote tukawaokoa wakiwa hai.


“Wakati tunaendelea kuzunguka, tukamuona abiria mmoja kwa mbali anaelea, tukamfuata na wakati wote huo meli na boti nyingine za waokoaji zilikuwa zikiwasili kwa kasi.


“Mungu ni mkubwa, kumbe yule kijana alikuwa ni mzoefu wa baharini, kwa hiyo alikuwa amekaa juu ya godoro huku anakula biskuti bila wasiwasi, yaani huwezi kuamini.


“Huyo kijana ambaye nilimkadiria kuwa ana umri wa miaka 28 hivi hatukumuokoa kwa sababu tuliona ana nguvu na anajiamini kwa hiyo, tukamwambia usiwe na wasiwasi tutakuokoa baadaye naye akakubali akatuambia ‘mimi sina shaka waokoeni wenzangu kwanza,” alisema Kilo.

Pamoja na matukio hayo, alisema wakati wanaendelea kuwaokoa abiria wengine, walimkuta mzee mmoja mnene aliyekuwa amekaa juu ya godoro mkononi akiwa na lundo la noti zilizokadiriwa kuwa zaidi ya Sh milioni tano.

“Huyo mzee hatukumuuliza chochote lakini mwingine tulimkuta akiwa na begi amelishika mkononi na tulipomuuliza kuna nini kwenye hilo begi akasema kuna kamera.

“Tukamwambia kama kuna kamera kwa nini usiitupe tu, kwa nini ung’ang’anie kamera wakati imeshaingia maji chumvi, huyo mzee akakataa, tukajua amejaza noti,” alisema.


Pamoja na maelezo mengi aliyotoa, alisema kazi ya uokoaji haikuwa ngumu kama ilivyotarajiwa kwa sababu wengi wao walikuwa na uzoefu wa majini.


Kwa mujibu wa Kilo, boti aliyokuwa amepanda iliokoa abiria 48 ingawa vile vile anasema haamini idadi ya watu 600 wanaoelezwa na Serikali waliokolewa katika ajali hiyo.


Maulid Machano ambaye ni kiongozi wa wavuvi katika eneo hilo, alisema baada ya ajali hiyo kujulikana wananchi wa Nungwi walikusanyika ufukweni mwa bahari kuangalia namna ya kuwaokoa wenzao.

“Mimi nilipata taarifa za tukio saa 7.00 usiku baada ya kupigiwa simu na mmoja wa abiria waliokuwa katika meli hiyo.


“Baada ya kupokea simu hiyo, nikawasiliana na wenzangu na baada ya dakika 15 wakazi wote wa Nungwi walikuwa wamefurika hapa baharini.


“Tukiwa hapo tukaanza kutafuta njia za kupata mafuta kwa ajili ya boti kwa bahati nzuri tukayapata japo tulichelewa kidogo kutokana na usumbufu tulioupata katika Kituo cha Mafuta cha SG Company,” alisema.


Wakati huo huo, wazamiaji kutoka Afrika Kusini waliotarajia kuanza kazi jana, inasemekana hawakuanza kazi jana kutokana hali mbaya ya hewa.


Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wavuvi wa eneo hilo zilisema wenyeji wa Nungwi waliokuwa wamekwenda baharini kwa ajili ya kutoa msaada kwa wazamiaji hao, walilazimika kurudi nchi kavu baada ya wazamiaji hao kutoonekana.


Hata hivyo, wakazi wa Nungwi, viongozi mbalimbali wa serikali na vikosi vya ulinzi na usalama walikuwa ufukweni mwa bahari kijijini hapo.


Katika eneo hilo, mahema yalikuwa yametandazwa kwa ajili ya kuhifadhia maiti na makundi ya watu yalikuwa katika vikundi vikundi.


Chanzo: Gazeti la Mtanzania, Septemba 14,2011

No comments:

Post a Comment