Wednesday, September 14, 2011

Alivyoshuhudia ndugu zake 32 wakifa baharini

MMOJA wa watu walionusurika katika ajali ya meli, MV Spice Islanders iliyozama katika Bahari ya Hindi visiwani Zanzibar, amesimulia namna alishuhudia ndugu zake 32 wakifa maji.


Akizungumza katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja , Shaame Faki Ally alisema walikuwa watu 36 kutoka familia moja.


Ally alisema safari yao ilianzia Dar es Salaam kuelekea Pemba kwenye harusi ya mdogo wao aliyemtaja kwa jina la Hadia Hassan na bwana harusi akimtaja kwa jina moja la Haji.


“Tulikuwa watu 36 wakubwa kwa watoto lakini walionusurika ni wanne tu, 32 wote wamefariki dunia katika ajali hiyo na kati ya watu waliofariki miili iliyoonekana ni saba waliobaki hawajaonekana mpaka sasa,” alisema Ally na kuongeza:


“Ingawa mimi ni mzima lakini mpaka hivi sasa sijui pakuanzia wala pa kutokea baada ya kutoka hospitali kwa sababu familia nzima imeteketea katika ajali hiyo.”


Ally ambaye ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuokelewa katika ajali hiyo alidai kuwa meli hiyo ilikuwa na watu wengi waliokuwa wametokea Dar es Salaam kuelekea Pemba.


“Meli ilikuwa imejaa na kumbuka wakati tunatoka Dar es Salaam tulikuwa watu wasiopungua 1,200 pamoja na mizigo na tulipofika Unguja ikapakia watu wengi hivyo kwa ujumla tulikuwa watu wasiopungua 2,000 ndani ya meli,” alidai.Akizungumzia safari ya kutokea Unguja kuelekea Pemba kabla ya meli kuanza kuzama, Ally alisema:


“Mimi nilikosa siti hivyo nikawa na kazi ya kuzunguka huku na kule na wakati mwingine nikishuka chini kwa ajali ya kuwanunulia maharusi vyakula na kila nilipokuwa nikipita niliwakanyaga watu au kuwaruka kutokana na umati mkubwa uliokuwa ndani ya meli.”


Alisema ilipofika majira ya saa sita usiku meli ikaanza kujaa maji, ghafla akawaona wafanyakazi wa meli pamoja na mabaharia wakizunguka na ndoo kwa ajili ya kuyachota, ndipo alipokimbia chini walipokuwa wenzake na kuwaeleza hali halisi.


Alisema kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya, alianza kuwaona mabaharia wakichukua majaketi na kuvaa kisha wakaanza kujitupa majini mmojammoja na wengine wakamfuata nahodha wa meli hiyo na kumtoa alipokuwa kisha wakamvisha jakati na kuondoka naye.


Alisema kuwa baada ya kuona tukio hilo, alianza kuwajulisha ndugu na jamaa kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo.


Tulikusanyika wote tukasali“Kwa kweli nilipoona hivyo nikajua sasa tumekwisha. Nikarudi tena chini nikakuta maji yameshajaa ndani ya meli ndipo tukakusanyika wanandugu wote tuliokuwa ndani ya meli pamoja na maharusi wetu tukaswali swala ya mwisho na kuambizana kuwa kila mtu ajiokoe mwenyewe na Mungu akipenda tutakutana popote pale iwe duniani ama peponi,” alisema Ally.


“Niliwakusanya watoto wote baada ya kuona wazazi wao wamechanganyikiwa na ukizingatia kwamba hawana uzoefu na masuala ya maji nikawapa godoro na kuwaambia kwamba walishikilie kwani ndilo itakalowaokoa.”


“Baada ya kuwapa watoto godoro, nikarudi kuwatafuta ndugu wengine lakini sikufanikiwa kuwaona tena ndipo nilipoamua kurudi juu kutafuta jaketi nikapata moja nikalivaa kisha nikarudi nilipowaacha watoto na kuungana nao. Wakati huo maji yalikuwa yameshajaa ndani ya meli.”


“Kidogo nikaokota mbao ambayo baadaye ilinisaidia kuvunjia moja ya dirisha la meli hiyo kwani wakati huo hata mlango ulikuwa hauonekani nikawapitisha watoto pamoja na mimi mwenyewe nikapita.”


“Nilipofika nje ya meli, nikakuta watu wengi wanaelea na majaketi yao wengine wakiwa wameshafariki dunia, kwa sababu yale majaketi kama hujui kuogelea hayawezi kukusaidia, isipokuwa ukifa huwezi kuzama badala yake utakuwa ukielea juu ya maji. Kadri muda ulivyozidi niliona watoto wakizidiwa na kuishiwa nguvu na mwishoni wote wakafariki dunia mbele yangu.”Muda wote akisimulia, Ally alikuwa akibubujikwa machozi…


“Baada ya kuona ndugu zangu wote wameteketea, ndipo nilipoanza kujiokoa mwenyewe na ilipofika saa 5:00 asubuhi, nikaona helikopta ikipita nikaanza kupeperusha shati langu kila wakati mpaka waliponiona na kuja kuniokoa.”


“Walipofika wakashusha kamba nikajitahidi kujivisha kwa shida kwani wakati huo wote hakuna hata kiungo changu kimoja kilichokuwa kinafanya kazi mwili ulianza kuchanika kwa sababu ya chumvi na baridi kali.”


Miongoni mwa walionusika alikuwamo mtoto wa miaka sita akiwa na dada yake mwenye umri wa miaka 12. Mama mdogo wa mtoto huyo, Mariam Hemedi alisema Said anaendelea vizuri na dada yake amesharuhusiwa kutoka hospitali.


Chanzo:Jackson Odoyo na Talib Ussi, Zanzibar

No comments:

Post a Comment