Friday, July 15, 2011

Washitakiwa kesi ya Magufuli waachiwa huru

Picha kwa hisani ya tovuti ya IPP media.


MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imewaachia huru washitakiwa 31 kati ya 36 waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kuvua samaki bila kibali katika Bahari ya Hindi, eneo la Tanzania.


Washitakiwa watano, kapteni wa meli Hsu Chin Tai (61), wahandisi wa meli ya Tawariq 1, Cai Dong Li (44) na Chen Rui Hai (34) na mawakala Zhao Hanquing (39) na Hsui Sheng Pao (55), wameonekana wana kesi ya kujibu.


Mahakama pia imeamuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuwarudishia hati za kusafiria na kuwaandalia utaratibu wa kuwarudisha makwao washitakiwa walioachiwa huru.


Imeamuru Jackson Toya (39), ambaye hana hati ya kusafiria arudishwe nchini Kenya.


Jaji Augustine Mwarija alitoa uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam.


Baada ya hukumu hiyo baadhi ya washitakiwa hao wakitokwa machozi ya furaha, wengine wakikumbatiana na hata kuzungumza Kiswahili, kwamba wamechoka kuishi Tanzania, hivyo ni bora warudi kwao.


Mmoja wa washitakiwa hao raia wa Vietnam, alisema kukaa kwake gerezani kumemwezesha kujifunza Kiswahili, amepata marafiki wa Kitanzania, waliokwenda kumjulia hali gerezani na kumpelekea chakula.


Kesi hiyo awali ilikuwa ikiwakabili washitakiwa 37 kutoka mataifa mbalimbali, lakini mmoja wao, Juma Juma, raia wa Kenya alifariki dunia wakati kesi ikiendelea.


Ilidaiwa kuwa, walikamatwa Machi 8, mwaka 2009, saa 6.00 usiku, katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ndani ya eneo la Tanzania, wakivua samaki bila kibali.


Jaji Mwarija amesema, amewaachia huru washitakiwa hao kwa kuwa hati ya mashitaka haielezi bayana ni washitakiwa gani walikuwa wakivua samaki, kwa kuwa wengine walikuwa wapishi na walikuwa wanatimiza majukumu yao.


Alisema, kapteni alikuwa msimamizi mkuu wa meli hiyo, hivyo pamoja na wenzake wanne wana kesi ya kujibu, watatakiwa kujitetea katika kikao kijacho cha mahakama.


Mawakili wa washitakiwa hao, Ibrahimu Bendera na John Mapinduzi, waliiomba mahakama iwapatie hati za kusafiria ili waweze kurudi kwao, kwa sababu zilitolewa mahakamani kama vielelezo.


Wakili wa Serikali, Biswalo Mganga, alisema, vyombo vinavyohusika ni lazima vifanye utaratibu ili waweze kuondoka na kurudi kwao.


Washitakiwa hao ni kutoka China, Indonesia, Kenya, Vietnam na Philippines.

No comments:

Post a Comment