Wazee wangu, chama chetu chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kimeamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha kiendelee kubakia chama kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.
Dhamira ya mwelekeo huo wa kufanya mabadiliko ya ndani ya chama chetu ilitangazwa rasmi na Mwenyekiti wetu Rais Kikwete wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, mjini Dodoma.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete aliyafananisha mabadiliko hayo na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya ‘Kujivua Gamba’.
Wazee wangu hatua ya kwanza ya utekelezaji wa azimio hilo na mwelekeo huo sahihi ilifanyika mjini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya CCM ambacho mimi nilikuwa mjumbe wake.
Wakati wa kikao hicho, wajumbe wote wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ya chama chetu wa wakati huo kwa kauli moja tulikubaliana kujiuzulu, lengo likiwa ni kumpa Mwenyekiti wetu fursa nzuri ya kufanya mabadiliko ya uongozi yatakayotoa nafasi ya kupata mwelekeo mpya wa Chama.
Wazee wangu, tulifanya hivyo tukionesha kuunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho bado naendelea kuamini kuwa ni mawazo sahihi na yenye mwelekeo thabiti ya Mwenyekiti wetu ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yakiakisi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa Oktoba mwaka jana.
Niliseme kwa maneno machache tu hili. Ingawa ni kweli kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umekirudisha madarakani chama chetu kwa kukipa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kiwango cha ushindi tulichopata kimeonyesha waziwazi dalili za wananchi kupunguza imani yao kwetu kuilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2005.
Tungekuwa ni chama cha siasa cha ovyo iwapo tungepuuza kupungua kwa kura za rais kutoka zaidi ya asilimia 80 tulizopata mwaka 2005 hadi kufikia aislimia 61 mwaka jana kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia 20 ya kura katika kipindi cha miaka mitano tu, hasa ikizingatia ukweli kwamba mgombea urais ni mtu yule yule.
Tungekuwa ni chama cha siasa kilichokosa umakini iwapo tungekaa pasipo kuchukua hatua zozote za kujiimarisha baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kuonesha wazi kukua kwa upinzani ambao umeongeza idadi ya wabunge na madiwani katika pande zote mbili za muungano.
Matokeo hayo ya uchaguzi ambayo hapana shaka yamekitikisa chama chetu yalitukumbusha wasia ambao tuliachiwa na Baba wa Taifa aliyesema; ‘Bila ya CCM Madhubuti Nchi Yetu Itayumba’.
Wazee wangu, kwa sababu ya kutambua ukweli kwamba hakuna haki isiyo na wajibu kama nilivyosema awali, mimi na wenzangu tuliokuwa katika Kamati Kuu tuliona ulazima, haja na umuhimu wa kukubali kwa kauli moja wito wa kututaka tujiuzulu ikiwa ni hatua moja ya kujipanga na kukijenga upya chama chetu.
KUJIVUA GAMBA KWAPOTOSHWA
Wazee wangu, kilichotokea baada ya kujiuzulu kwetu kila aliye ndani na nje ya chama chetu amekisikia na anakifahamu. Chama kilipata safu mpya ya uongozi iliyotokana na kuundwa kwa Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wetu mpya, Mhe. Wilson Mukama, na Kamati Kuu iliyokuwa na sura tofauti na ile ya awali.
Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya chama chetu, ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu tukiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye.
Mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kilichagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu na kuidhinisha uundwaji wa Sekretarieti mpya, dhana ya kujivua gamba ambayo naamini Mwenyekiti wetu aliianzisha kwa nia njema ilianza kuenezwa ikichukua tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.
Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mhe. John Chiligati, na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Mhe. Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku tisini wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.
Wazee wangu, baada ya kushinikizwa sana na vyombo vya habari wawataje kwa majina wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao ni wajumbe wa NEC na ambao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao, wajumbe hao wa Sekretarieti walikwenda mbele zaidi.
Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walikuwa wakilengwa na maamuzi hayo.
Wazee wangu, nilishangazwa na kushitushwa na namna porojo na fitina za kisiasa zilivyofinyangwa kwa mara nyingine tena baada ya kusikia jina la mbunge wenu ambaye ni mimi, likitajwa kuwa miongoni mwa yale matatu ya viongozi waliokuwa wakitakiwa eti kupima wenyewe na kisha kuchukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya NEC katika kipindi cha siku tisini.
Niliseme hili mapema. Mshangao na mshituko wangu haukusababishwa na kutajwa kwa jina langu, la hasha, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.
Pili, nilishangazwa na kushitushwa na hatua ya viongozi wa chama changu ambacho nimekitumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa kufanya juhudi kubwa hata kukivisha kikao kitukufu cha NEC uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya kisiasa yaliyo ndani ya CCM kwa upande mmoja na propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.
Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria ukiachilia mbali ushahidi wa wazi umeshathibitisha kwamba ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.
Wazee wangu, nyinyi ni mashahidi kwamba, mbali ya mimi mwenyewe kujitokeza kupitia vyombo vya habari na kueleza wazi kwamba sijapata kujihusisha katika vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au vya rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaonihusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa.
Wazee wangu, ni wazi kwamba kama chama chenye siasa chenye dhamana ya kuwaoongoza Watanzania kutoka katika lindi la ufukara, maradhi, matatizo ya makaazi na mengineyo siku zote tunapaswa kuwa makini katika kuhakikisha kwamba changamoto za kuwaongoza na kuwakomboa wananchi waliotupa dhamana hazitikiswi na mawimbi ya matakwa ya nyakati ama ya vyombo vya habari au wapinzani wetu wa kisiasa walio nje ya CCM.
Ni kwa sababu ya kulitambua hilo na hasa kuyatambua madhara yanayoweza kukipata chama chetu na nchi yetu iwapo tutaendekeza siasa za kupakana matope pasipo na sababu za msingi, kuchafuana kusikokoma na kulipizana kisasi ndiyo maana nimeona nitumie fursa hii kuzungumza nanyi wazee wangu ili kuweka kumbukumbu sahihi.
No comments:
Post a Comment