MSIBA tena! wasanii wengi wa bendi ya muziki wa Taarab la Five Stars Modern Taarab wamekufa katika ajali iliyotokea Morogoro.
Kwa mujibu wa habari kutoka huko, watu 13 wamekufa na wengine 9 wamejeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea jana saa 2 usiku katika barabara ya Morogoro- Iringa.
Inadaiwa kuwa watu 12 walikufa papohapo katika eneo la ajali kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Miongoni wa waliokufa katika ajali hiyo ni kiongozi wa bendi hiyo, Nassoro Madenge, na wasanii maarufu wa taarab Tanzania akiwemo Issa Kijoti.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la ajali, uzembe wa dereva wa gari lililokuwa limebeba wasanii aina ya Toyota Coaster, aliyetajwa kwa jina la Chala ndiyo uliosababisha ajali hiyo.
Inadaiwa kuwa, Chala alitaka kulipita lori lililokuwa limeegeshwa lililokuwa limebeba mbao, na wakati anafanya hivyo, ghafla aliona lori lililokuwa linakuja mbele yake, hivyo akaona azuie kugongana uso kwa uso, akaligonga lori kwa nyuma, na coaster likapinduka.
Inadaiwa kuwa watu wote waliokuwa upande wa kushoto wa gari hilo wamekufa.
Muda mfupi uliopita nimepata taarifa kwamba, kati ya watu 9 waliojeruhiwa, wanne hali zao ni mbaya sana.
Wasanii waliokufa walikuwa wanatoka kufanya maonesho ya muziki katika mikoa ya nyanda za juu kusini wanarudi Dar es Salaam.
Muda mfupi uliopita, msanii maarufu wa taarab nchini, Khadija Kopa, amesikika akilia kwa uchungu.
Kopa yupo Dar es Salaam, lakini ilikuwa nae aende kwenye safari hiyo lakini alishindwa kwa sababu ya majukumu mengine.
Kwa mujibu wa Kopa, ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupoteza wasanii wengi kwa mara moja na ameshauri lifanyike tamasha ili kuzichangia familia za marehemu.
Mmoja wa wasanii waliokuwa kwenye gari lililobeba wasanii, Ally J, amekaririwa akisema kuwa, dereva wao alikuwa anakwenda kwa kasi, walimwambia lakini hakuwasikiliza.
Mmoja wa wasanii waliokuwa kwenye gari hilo amekaririwa akisema, kitu cha mwisho anachokumbuka kabla ya ajali hiyo ni sauti kali ya msanii mwenzake , Issa Kamongo , akisema 'Chala unatuua'.
Kamongo amejeruhiwa na nimearifiwa kwamba, ameruhusiwa kutoka hospitali.
Kuna taarifa kwamba miili ya marehemu ipo njiani kuletwa Dar es salaam, inatarajiwa kufika saa tisa alasiri katika Hospitali ya Temeke.
No comments:
Post a Comment