Tuesday, March 22, 2011

Inasikitisha, pole Watanzania

AJALI iliyotokea jana usiku na kuua zaidi ya wasanii 10 wa bendi ya taarab ya Five Stars Modern Taarab imeacha pengo, huzuni, majonzi, simanzi kwa Watanzania hasa wadau wa muziki, mashabiki wao, na familia zao.
Jumla ya watu 13 wa bendi hiyo wamekufa wakiwemo wanaume 8 na wanawake 5.
Miili ya marehemu ipo njiani kuletwa Dar es Salaam, inatarajiwa kufikishwa leo alasiri katika Hospitali ya Temeke.
Mmoja wa wadau wakubwa wa muziki nchini, Asha Baraka amesema, Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood, amejitolea magari kusafirisha miili ya marehemu hao wengi wao wakiwa vijana.
Wengi waliokufa ni Waislamu, hivyo huenda watazikwa leo au kesho na kwa taratibu za dini hiyo miili hiyo haitaagwa.
Asha Baraka amesema, wengi waliokufa ni vijana waliokuwa wanaanza maisha hivyo wameacha pengo katika familia zao.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, takribani wapiga vyombo wote wa Five Stars Modern Taarab wamekufa.
Amesema, wengi wa wanamuziki waliokufa, kabla ya kujiunga Five Stars walikuwa Jahazi Modern Taarab linaloongozwa na Mzee Yusuf.
Miongoni mwa waliokufa ni Hamisa Mipango, Issa Hassan Kijoti, Husna Mapande, Sheba Juma, Ramadhani Kinyoya, Haji Mzaniwa, Omary Tally, Tizo Mgunda, na mcheza shoo Maimuna Makuka.
Msanii maarufu wa Taarab, Hammer Q alikuwa katika safari hiyo lakini alishuka Iringa Mjini akasema angekuja Dar es Salaam leo.
Hivi sasa Msanii huyo yupo njiani katika basi kuja Dar es Salaam kuwahi mazishi ya wenzake.
Msanii mwingine wa kundi hilo, Joha Kassim, hakwenda kwenye ziara hiyo.
Taratibu za mazishi zinaratibiwa katika ukumbi wa Ikweta Grill, Temeke mkoani Dar es Salaam.
Watu wakifika pale wamuone mmiliki wa ukumbi huo ambaye pia ni kiongozi wa Zanzibar Stars, Ferouz ili waelekezwe taratibu za mazishi na maziko.

2 comments:

  1. Ni kweli ni pigo kubwa. Marehemu na wastarehe kwa amani peponi. Amina

    ReplyDelete
  2. INNA LILAH WAINA ILLAHI RAJUUN
    INSHALLAH MWENYEZI MUNGU ATUFANYIE WEPESI WAFIWA WOTE KTK KIPINDI HKI KIGUMU CHA KUONDOKEWA NA WAPENZI NDG NA JAMAA ZAO

    ReplyDelete